iturujia ya Neno la Mungu inaweka mbele ya macho ya waamini mateso na mahangaiko katika maisha ya mwanadamu na jinsi imani inavyoweza kupyaisha matumaini kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Taabu na mahangaiko ya mwanadamu ni matokeo ya dhambi. Katika shida na magumu ya maisha, waamini wajifunze kumtumainia Kristo Yesu katika maisha yao.

Na Padre. Joseph Herman Luwela-Kibarua wa Kristo-Vaticani Roma-Italia
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 13 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani inayopyaisha matumaini kwa Kristo Yesu. 

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji karibu katika tafakari ya dominika ya 13 ya mwaka B wa Kanisa. Injili leo imebeba viashiria vya majanga, lakini imani anamatumaini vilaleta jibu na utatauzi wa changamamoto mfano: kuugua na kufiwa, homa za wanetu huondoa amani na utulivu. Kwa wayahudi msichana aliingia umama alipofika miaka 12 na siku ya kwanza na hapo aliweza kuchumbiwa. Hivi kifo cha binti huyu katika umri ule ni janga la uhakika. Baba yake, Yairo, anaomba msaada kwa Kristo, ni mkuu na msimamizi wa shughuli za Sinagogi hivi kuja kwa Yesu kunatupa mambo kadhaa… UFAFANUZI: Mosi, mtazamo wake mbaya juu ya Yesu uliyeyuka mbele ya shida ile. Wakuu wa Masinagogi walimwona Yesu mleta fujo, anaponya siku za sabato na hazingatii mapokeo wakamdharau, amesahau yote. Mara nyingi tumepata msaada kutoka kwa tusiowadhania au tuliowadharau. Tukumbuke kila mmoja ni wa muhimu hata kama anaonekana duni machoni petu. Pili, hadhi na ukuu wake vilisahaulika, akajitupa miguuni pa Kristo kwa unyenyekevu. Nasi mara kadhaa tumejiona tuna hadhi kiasi cha kukosa unyenyekevu na hivi kutojibiwa sala zetu. Tatu, marafiki na wakuu wenzake walisahaulika, akabaki peke yake, akajitambua na kusaidiwa. Mara kadhaa tunapaswa kujitenga na ushawishi na mitazamo ya makundi ya watu na kubaki peke yetu na Kristo, tutasaidiwa.

Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha mapya

Njiani mwanamke mwenye kutoka damu anajitokeza na kuzidi kuipamba Injili hii izidi kufana. Amehangaika sana. Pamoja na maumivu, mgonjwa wa hivi alikuwa najisi, hakushiriki makusanyiko ya ibada na ya kijamii akatengwa na Mungu na watu (Law 15:25-27). Aliuza vitu vyake kugharamia matibabu lakini hakusaidika, akabaki na msiba miaka 12, oh! ni shida kubwa. Katika kukata tamaa, akasikia habari za Yesu akapata tumaini jipya kuwa hatimaye shida yake imepata jawabu. Lakini alipoutafakari ugonjwa wake na kwamba Yesu hana nafasi ya faragha, moyo ulimsinyaa, akajikunyata na kujihoji ‘nitamuonaje?’ kujieleza mbele ya watu shida kama hii, aibu! wangemuonaje? Hasa wanaume, vijana na watoto, alihofu wangemcheka na kumdhihaki katika unajisi wake. Akapata wazo. Plan A ikifeli ni lazima B itumike na lengo lifikiwe, usirudi nyuma, kuketi, kushusha pumzi na kusema ‘imeshindikana’ daima kwako iwe ‘ bado nusu kujaa na sio nusu kwisha’. Akajitosa na kugusa upindo wa vazi la Yesu, chemchemi ya damu ikakauka akapona shida yake, alleluia. Katika tukio hili kuna watu aina 4. Mosi, Kristo. Analalamika ‘ni nani aliyenigusa?’ anaonja nguvu zimemtoka. Kumbe gharama ya uponyaji ni sehemu fulani ya uhai wetu. Ukristo unatudai kujitoa na kupungukiwa nguvu, sehemu yetu ipungue kwa faida ya wenzetu, itumike kama sadaka, iteketee kama mshumaa ili kuangaza. Wazazi hutumia nguvu ndipo muujiza hufanyika na mtoto kupatikana, wakati unapotimia ni lazima nguvu zimtoke mama ndipo ajifungue salama. Ili kusaidia wahitaji, kupenda na kusamehe tunadaiwa nguvu itutoke. Huyu ndiye Yesu, anaonja nguvu zimemtoka kwa tendo la mama huyu.

Kristo Yesu ni faraja na tumaini kwa wale waliovunjika moyo!

Kundi la pili ni wafuasi wa Yesu… wanaonesha umasikini wa milango 5 ya fahamu kufikia ukweli wa kiroho. Macho yao yamedanganywa na umati hivi Yesu anapouliza ‘nani aliyenigusa?’ wanamshangaa ‘Ee Bwana vipi? Ona watu wanavyokusongasonga nawe unauliza ni nani aliyenigusa?’ Nasi hudanganyika na kuhangaikia vinavyovutia machoni, vitamu mdomoni, laini kuvigusa na vinapendeza kuvisikia lakini kimsingi si vya muhimu kwa ufalme wa mbinguni. Mtu wa tatu ndiye huyu mama… Kwake tunajifunza nafuu ya kitubio na maungamo. Aliona ngumu kujieleza lakini Yesu alipouliza akakosa namna, akaungama na kupewa maneno ya upole na upendo ‘binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani…’ Mkristo utamani maneno mazuri hivi.. hofu, mashaka na kutetemeka vikaisha, anapata amani, anajaa furaha, hakuna msiba tena… kuna nguvu ya kutisha katika kitubio, upatanisho, ahueni, inaondoa mizigo na kuleta wepesi. Mwisho ni watu waliomsongasonga.. walimfuata, walimuona, walimsikia, hawakumgusa walimsonga tu.. aliyemgusa kiuhalisia ni yule mama, kwa nini? alimgusa kwa imani. Inawezekana nasi tunaomsongasonga Yesu tunapokuja Kanisani, JNNK, vyama vya kitume na sala, katika Ekaristi lakini maisha yetu hayabadiliki, ugonjwa hauponi tunaendelea kutaabika, hii ina maana bado hatujagusa walau mavazi yake, tumekutana nae juu juu tu, ameingia masikioni na sio mioyoni mwetu.

Bikira Maria ni faraja na matumaini ya Kanisa linalosafiri hapa duniani

Wanafika watumishi wa Yairo na kumkatisha tamaa, ‘binti yako amekufa kwani kumsumbua mwalimu?’ hawana imani. Yesu anasisitiza ‘usiogope, amini tu!’ Nawe mkristo katika sintofahamu ya maisha yako neno ni hilohilo la Yesu, ‘usiogope amini tu!’.. wanafika nyumbani, anamfufua na wote wanashangaa. Mkristo sema moyoni mwako ‘nikiyagusa mavazi yake tu nitapona…’ Upone yote yanayokuweka mbali na Mungu na wenzako. Mungu hataki ufe anataka uishi, ni Mungu wa walio hai, sio wa waliokufa. Somo I (Hek 1:13-15,2:23-24) linasema ‘Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea…’ tuna mengi yanayotuua, tunahitaji kuyagusa mavazi ya Yesu. Tuguse mavazi ya Yesu walegevu wa kusali, tunaosali tumetawanya mawazo, tunaosali huku tunachukiana, vinyongo, uongo, tunaishi maisha bandia tofauti na tulivyo, tumepungukiwa utukufu wa Mungu. Ziguse mavazi ya Yesu familia zisizoishi upendo na maelewano, wahusika wake sio wakweli. Utandawazi umezitafuna zimebungua. Simu za viganjani zimeleta kutoaminiana, kutokuwa wakweli wa wapi tulipo na zikiunganisha wengi katika mtandao wa mahusiano yasiyo na afya njema… Badala ya sala za jioni, tunatulizana mbele ya Tv tukitazama mpira, tamthilia, habari na burudani. Hakuna udhibiti wa nini tuone kinatufaa na nini tuache hakitufai. Sera za uzazi na matumizi ya vidhibiti mimba vinamong’onyoa utakatifu wa ndoa, matumizi yanazidi kipato, wengi tunajali kazi kuliko mahusiano ya kimapendo, shime tuyaguse mavazi ya Yesu tupate kupona. Kristo na atutazame, tumsikie mioyoni mwetu ‘baba, mama, shangazi, mjomba, kaka, dada, mtoto, rafiki… imani yako imekuponya enenda zako kwa amani.’