Mapadre Wekezeni Zaidi Katika Huduma Kwa Wazee na Vijana Huko Maparokiani
Papa Francisko na Mapadre 160 kutoka Jimbo kuu la Roma, hivi karibuni walifanya mazungumzo ya faragha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian wa Don Bosco, Roma. Tema: Ushuhuda wa ukarimu Parokiani; Ulinzi na tunza ya wazee na vijana wanaoogelea katika changamoto za maisha; biashara haramu ya silaha, vita na masuala ya kisiasa; malezi na makuzi ya Majandokasisi Seminarini; matatizo, shida na changamoto za Mapadre katika maisha na utume wao.
NA Padri Joseph Herman Luwela-Kibarua wa Kristo-Vatican Roma
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu wito na maisha ya Daraja takatifu ya Upadre anapenda kukazia sana umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa sababu Kristo Yesu ndiye chemchemu ya upendo kwa waja wake. Wakleri wanakumbushwa kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu, wao kimsingi ni: waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Huu ndio urithi unaojikita katika Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa. Ni ukweli ambao wakleri wanapaswa kuumwilisha katika maisha na utume wao kwa njia ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Padre daima anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, Ibada kwa Bikira Maria inawawezesha wakleri kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, ili kweli waweze kuwa wafuasi na mitume hodari wa Kristo Yesu kwa kusikiliza na kutenda kama alivyokuwa Bikira Maria. Daima amekumbusha kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, ni watu wanaopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwani wao ndio walengwa hasa wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, amekutana na kuzungumza na Mapadre waliohitimisha maisha na utume wao katika Daraja Takatifu ya Upadre katika kipindi cha kuanzia miaka 11 hadi miaka 39. Hiki ni kipindi kinachowapatia Mapadre fursa ya “kuchakarika zaidi” katika maisha na utume wao wanapotekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
atika mazungumzo haya ya faragha kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Mapadre 160 kutoka Jimbo kuu la Roma, yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian wa Don Bosco, Roma, kati ya tema walizojadili ni: Ushuhuda wa ukarimu Parokiani; Ulinzi na tunza ya wazee na vijana wanaoogelea katika changamoto za maisha; biashara haramu ya silaha, vita na masuala ya kisiasa; malezi na makuzi ya Majandokasisi Seminarini; matatizo, shida na changamoto za Mapadre katika maisha na utume wao. Padre Lorenzo Milani, Mkuu wa nyumba ya kitawa ya Barbiana katika maisha yake alijiwekea utamaduni wa kukimbilia mara kwa mara katika kiti cha huruma ya Mungu ili kuomba toba na msamaha wa dhambi zake kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya huruma ya Mungu na Mama mpendelevu kwa watoto wanaokimbilia huruma na tunza yake ya kimama. Ni kiongozi ambaye alibahatika kuwa ni mwalimu na mlezi wa vijana; tunu msingi alizorithishwa kutoka katika familia yake ambayo haikuwa na imani na wakati mwingine, ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa Mapadre. Ni tabia ambayo aliibeba katika maisha yake, kiasi kwamba, hata wakati mwingine alikuwa ni mgumu na wengi walishindwa kumwelewa hata baada ya toba na wongofu wake wa ndani kunako mwaka 1943, wakati anatekeleza dhamana na wajibu wake wa kichungaji kama Padre. Haya ni mambo yanayoweza kujionesha katika maandiko yake mintarafu mfumo wa elimu, upendeleo kwa maskini pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha uhuru wa dhamiri. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kulipenda na kulithamini Kanisa hata kama limejeruhiwa vibaya. Lakini elimu inayotolewa na Kanisa inawasaidia watu kuwa na upeo mpana kuhusu uhalisia wa maisha kwa kufungua akili na nyoyo zao, kiasi kwamba, wanaweza kuwa ni jasiri kukabiliana na ukweli wa maisha.
Shuleni watu wanajifunza kwanza kabisa: Mambo msingi kwani shule ni mahali ambapo mtu anajifunza kujifunza na baada ya kujifunza anaendelea kujifunza zaidi kwani elimu haina mwisho. Huu ni ushuhuda wa wema na upendo kwa wanafunzi wake aliotamani kuwapatia utu na chachu ya upendo kwa Kristo na Injili yake; kwa Kanisa na Jamii, huku akitamani na kuota kwamba, shule iwe ni hospitali wazi katika uwanja wa vita, ili kuwaokoa na kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kuwapatia ujuzi, kufahamu na kuzungumza kwa weledi, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao msingi. Haya ni mambo ambayo Padre Lorenzo alipenda kuyatumia hata wakati wa mahubiri yake na maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali za Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Parokia ziwe ni mahali pa kumwilisha huduma ya ukarimu kwa watu wote wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, vijana na wazee wanahitajiana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni unaowakutanisha vijana na wazee, ili kukoleza moyo wa majadiliano. Bila mchakato wa majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya, maisha na historia ya mwanadamu vitagota mwamba na maisha hayataweza kusonga mbele hata kidogo! Majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ni changamoto katika ulimwengu mamboleo. Wazee wanayo haki ya kuota ndoto, huku wakiwaangalia vijana. Na vijana kwa upande wao, wanayo haki na ujasiri wa kinabii, huku wakichota hekima na busara kutoka kwa wazee. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa, anawaalika wazee na vijana kujenga utamaduni wa kukutana na kuzungumza kwa pamoja, mwelekeo huu utakuwa ni wa manufaa kwa makundi yote mawili.
Baba Mtakatifu amegusia changamoto wanazokabiliana nazo vijana wa kizazi kipya: Upweke hasi unaowapelekea kutumbukia katika ugonjwa wa sonona na matokeo yake, kuna ongezeko kubwa ya idadi ya vijana wanaotema zawadi ya uhai kwa kujinyonga, baada ya kushindwa kugundua maana na umuhimu wa maisha. Upweke hasi unaweza kuwakumba hata Mapadre, kumbe, wanapaswa kuwa makini sana katika maisha na utume wao. Kanisa ni shuhuda wa unabii. Baba Mtakatifu amegusia pia kuhusu vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia lakini zaidi: kati ya Ukraine na Urusi, Palestina na Israeli, Congo DRC na Myanmar. Haya ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani inayoendelea kusababisha umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia; ni biashara inayowaletea wahusika faida kubwa inayonuka damu. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu hatari ya kuwaruhusu vijana wenye mwelekeo na tabia ya ushoga kuingia Seminarini kwani hii ni hatari sana kwa maisha na utume wa Kanisa, ni muhimu kufuata na kuzingatia mwongozo wa malezi na makuzi ya Kipadre uliotolewa na Baraza la Kipapa la Wakleri.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Aprili 2024 alimteuwa Kardinali Angelo De Donatis kuwa Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume na hivyo kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Kardinali Mauro Piacenza. Kunako mwaka 2014 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuongoza mafungo ya Kipindi cha Kwaresima kwa Baba Mtakatifu Francisko na waandamizi wake wakuu. Tarehe 14 Septemba 2015 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma na kuwekwa wakfu tarehe 9 Novemba 2015. Baba Mtakatifu Francisko alisema, Kristo Yesu katika utekelezaji wa utume wake hapa duniani aliwachagua Mitume pamoja na waandamizi wao ili kuendeleza mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote, wakiwa chini ya Mchungaji mmoja pamoja na kuendelea kuwatakatifuza, kuwafundisha na kuwaongoza watu wa Mungu kuelekea kwenye uzima wa milele. Baba Mtakatifu alimkumbusha Kardinali Angelo De Donatis kwamba, ameteuliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya mambo yamhusuyo Mungu; kwa ajili ya huduma kadiri ya mfano wa Kristo mchungaji mwema na wala si kwa ajili ya kuwatala watu. Alimtaka kutangaza na kushuhudia Injili na Mafundisho ya Kanisa. Mahubiri yawe ni chemchemi ya neema kwa watu wa Mungu, ili waweze kuwa wema na watakatifu zaidi. Awe ni mchungaji na mlezi mwema wa Mapadre na Majandokasisi pamoja na kuendelea kuonesha upendo kwa waamini wote, hususan maskini, wagonjwa na wote wanaohitaji msaada wa Kanisa.
Kardinali De Donatis anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwamini na kumkabidhi madaraka ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu tangu tarehe 9 Novemba 2015. Katika kipindi chote hiki, Kardinali De Donatis anasema, amegundua kwamba, hii ni familia inayopaswa kupendwa na kuendelea kukua na kukomaa katika utii na udugu wa kibinadamu. Kipaumbele cha pekee ni: Kulisikiliza, Kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kufanya mang’amuzi katika ngazi ya mtu binafsi na yale ya kijumuiya, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu Jimbo kuu la Roma. Hii ni sehemu ya ujumbe uliotolewa na Kardinali De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, baada ya uteuzi huu mpya, tayari kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza Kardinali Angelo De Donatis kwa utume wake mpya kwani sasa ameitwa kuwa ni kielelezo cha Uso wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Mwenyezi Mungu aliwakirimia wanadamu Roho wake ili wapate ustadi, ufahamu na ujuzi katika kila kazi. Kwa hiyo sayansi na teknolojia ni bidhaa nzuri za uwezo wa ubunifu wa wanadamu na kwamba, teknolojia ya akili mnemba hutokana hasa na matumizi ya uwezo huu wa kazi ya uumbaji uliotolewa na Mwenyezi Mungu.
eknolojia ya akili mnemba ni chombo chenye nguvu sana kinachotumika katika medani mbalimbali za shughuli za mwanadamu. Kutoka katika dawa hadi katika ulimwengu wa kazi; utamaduni, mawasiliano, elimu na siasa na kwamba, matumizi ya teknolojia ya akili mnemba yanaathari zake katika maisha ya mwanadamu, mahusiano na mafungamano yake kijamii na hata jinsi ya kufikiria utambulisho wao kama wanadamu. Suala la teknolojia ya akili mnemba huchukuliwa kama utata, kwani kwa upande mmoja hutoa msisimko unaowezekana na wakati mwingine husababisha hofu kwa matokeo ambayo hutangulia. Kumbe hapa kuna hisia ya maendeleo makubwa yanayotokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba na wakati huo huo, woga unashamiri kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 wakati akishiriki mkutano wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7. Huu ni wito wa kutafuta, kujenga na kudumisha amani sanjari na ubinadamu katika enzi ya akili mnemba. Baba Mtakatifu ameshiriki mkutano huu kwa mwaliko kutoka kwa Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni.