Tafakari Dominika 21 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani, Matumaini na Utashi Kamili “Je nanyi pia mwataka kuondoka?”

Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku ule alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele.”

Na Padre Joseph Herman Luwela, – Vatican.Roma, Italia

 Mambo msingi ni imani, matumaini na utashi thabiti wa kuambatana na Kristo Yesu mwenye maneno ya uzima wa milele. 

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican,Leo Mwenyezi Mungu anasema nasi kupitia wajumbe wa Neno lake. Anatujenga kwa mafundisho ili tumwendee katika utumishi mwema kwa uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu kweli na mtu kweli katika maumbo ya mkate na divai. “Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku ule alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake Azizi. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele.” (KKK 1323). Leo kila mmoja ajiweke mahali pa Mitume, Kristo anatuuliza ‘Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka? Baada ya Yesu kutoa hotuba ndefu juu ya kuutambua, kuupokea, kuula mwili wake na kuinywa damu yake wengi waliona ni neno gumu wakarudi nyuma wasimfuate tena. ‘Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena, basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?’ (aya 66-67)Swali hili linatuhusu pia katika kizazi chetu. Wengi wetu, mimi na baadhi yenu hatuandamani tena na Kristo, ndugu wengi wamerejea nyuma kwa kuasi imani na kuambatana na imani nyinginezo. Wengine wamepata mitazamo mipya, mafundisho tofauti, wapo waliojikita katika uzalishaji kiasi cha kumwacha Yesu, wengine wameamua kujivuta na kufuata mashauri yao wenyewe, wapo waliozama katika siasa na kutokuwa na mpango na mambo ya Mungu, wapo waliobobea katika ulevi na dawa za kulevya. Uwepo wa fidia na viinua mgongo, bima za afya, za magari na za maisha, madaraka na mishahara ya uhakika, afya njema na akili nyingi vimepelekea kujiona tupo salama, tunaweza kutembea peke yetu.

wende kwa nani Wewe unayo maneno ya uzima wa milele!

UFAFANUZI: Kristo hakusema ‘Wewe Petro na wenzako nawaomba sana, tafadhali, msiniache peke yangu, kaeni nami msiondoke!’ Hamshawishi mtu kubaki naye, halazimishi kumfuata lakini anadai imani na matumaini kwake. Swali hili lituguse sote ili tufanye maamuzi ya kuondoka au kumfuata. Mitume 12 walijibu changamoto hiyo wakabaki waaminifu, wanaonesha hisia zao kwake. ‘Bwana! Twende kwa nani, wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe mtakatifu wa Mungu’ (aya 68-69).  Uhuru huu umejitokeza pia katika somo I (Yos 24:1-2a, 15-18b) ambapo Yoshua amewakusanya Israel na kuwakumbusha historia yao. Anawataka waamshe ahadi na viapo vyao kwa Mungu. Waisrael, kama mitume, wananjibu kwa busara ‘hasha! tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine’. Yoshua anatuambia na sisi ‘chagueni hivi leo mtakayemtumikia’ Kristo anatuuliza ‘Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?’ Nawaalika tuchague na tujibu kwa busara. Petro alitambua kuwa ni Yesu tu ndiye mwenye maneno ya uzima kwa vile alikuwa karibu naye. Nasi tupo karibu naye, tulijibu kwa busara tulipobatizwa na tukaahidi kumtumikia. Tusimwache hata mara moja, Yeye ni nuru nje yake ni giza litishalo. Kristo ni uzima, nje yake ni mauti. Kristo ni nguvu yetu, nje yake ni unyonge na udhaifu. Kristo ni upendo wetu, nje yake ni chuki, hila na malumbano. Kristo ni njia yetu, nje yake ni upotevu… Kristo ni kila kitu.

Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.

Tunapoyatafakari maisha yetu hitaji la kuamua kwa busara na hivi kumfuata na kumtumikia Bwana. Maneno ya Yoshua ‘ninyi chagueni wa kumtumikia lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana’ yanatupatia zawadi ya baba wa familia mwenye msimamo na maamuzi imara juu ya hatima ya nyumba yake, ‘mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana…’ Maneno haya yanatoa picha ya baba kama kichwa cha familia anayeongoza mambo yote, maendeleo, ustawi na mafanikio. Hata wote watamwacha Bwana lakini wote katika katika nyumba ya huyu baba watamwabudu Mungu aliye hai. Jambo hili lisifanyike kwa nguvu bali kwa hekima na uongozi wa Roho Mt. kwa sababu jamii sasa imani nyingi na wengi, imesema Injili, tunarejea nyuma tunamwacha Kristo. Misingi iwekwe mapema na msimamo wa baba ujulikane… nampenda baba mwenye ujasiri na uwezo wa kusema kama Yoshua ‘ninyi chagueni wa kumtumikia lakini mimi na nyumba tutamtumikia Bwana.”Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka? Bwana twende kwa nani? Kumfuata Yesu ni kuyaishi mausia yake. Somo II (Efe 5:21-32) linafafanua namna iwapasayo wanafamilia katika ufuasi wao kwa hekima ya kimungu. Mt. Paulo anaagiza wake wawatii waume, waume wawapende wake zao. Huwezi kumpenda mtu usiyemtii hivyo utii unawahusu pia wanaume. Baba anaposema ‘mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana’ anakuwa msemaji tu wa yale yaliyojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi wa pamoja. Tupo akina baba tunaoamua mambo bila kuwashirikisha wenzi wetu, hawa japo wamebatizwa wangali bado na kaupagani kadogo.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Nimependa sentensi hii kutoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume ‘ampendaye mkewe anajipenda mwenyewe’ kwa hiyo anayempiga mkewe, anajipiga mwenyewe na kujipiga mwenyewe ni kukosa akili. Muhimu ni staha, utambuzi na uvumilivu. Kufunga milango/mdirisha na kuvuta mapazia na hivi kuiacha nje hewa yoyote mbaya inayoweza kuharibu nyumba yetu. Kuishi Neno la Mungu, kusali na kutoa sadaka kwa masikini. Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka? Hapana hatuondoki. Ikiwa hivyo basi tutunze haki na amani kwa vile Yeye ni Bwana wa amani naye ni mwenye haki, usimuonee jirani yako hata akiwa tofauti nawe. Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka? Bwana twende kwa nani, wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Wayahudi wanamjibu leo Yoshua, ‘La hasha, tutamtumikia Bwana’… utumishi huo ni huduma ya kiinjili na kimapendo. Kusudi sote kwa umoja tumtumikie Mungu tunapaswa kuuishi umoja, umoja upo katika kusaidiana kuinuka na sio kukandamizana. Tuwainue walioanguka, tuwagange wagonjwa, tuwafunge majeraha walioumia kwa namna mbalimbali. Lakini hatuwezi kuinuana kama sote tupo chini. Mtu aliyeanguka hawezi kumsaidia aliyeanguka ila aliyesimama. Tusimame kwanza katika kitubio, turekebishe maisha yetu, turudi kundini kushiriki Mmwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu halafu tutaweza kuwasaidia ndugu zetu. Tuombe neema ya kuyaishi mapenzi ya Mungu. Kristo anasema leo kuwa ‘roho ndio itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima’ tuyazingatie tupate kuishi.

Similar Posts