|

Tafakari Dominika ya 16 ya Mwaka B wa Kanisa: Umuhimu wa Likizo: Sala, Neno na Matendo ya Huruma

Njooni kwangu mpumzike

Likizo ni nafasi muafaka ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu Fumbo la maisha ya binadamu, ili kubainisha ikiwa kama maisha yana alama na chapa ya uwepo endelevu wa Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza waja wake katika mapito ya maisha

Na Padre Joseph Herman Luwela, – Vatican.Roma Italia

Likizo ni kipindi cha kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani

UTANGULIZI: Hili ni neno la faraja kutoka kwa Kristo lenye ladha ya kuwajali mitume baada ya ripoti yao ya kazi aliyowatuma na uchovu waliokuwa nao, “vema wanangu, hingereni kwa kazi, hebu tuache kwanza kila kitu twende tupumzike kidogo”, haoo wakaondoka zao! Upande wa pili wa ziwa watu ni wengi tena wametawanyika tu.. Kristo anasahau mapumziko aliyopanga, anawahurumia na kuwafundisha. Huyu ndiye Yesu, mwanzo anawahurumia mitume wamechoka na sasa anawahurumia watu waliotawanyika bila mwongozo, hajitazami wala hajihurumii mwenyewe, kwake furaha na usalama wa wanaomzunguka ni muhimu kuliko chochote. Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, inapaswa kuwa na uhusiano na sehemu nyingine za maisha ya binadamu. Likizo iwe ni fursa ya kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha. Kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili! Likizo ni nafasi muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu Fumbo la maisha ya binadamu, ili kubainisha ikiwa kama maisha yana alama na chapa ya uwepo endelevu wa Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza waja wake katika mapito ya maisha. Likizo ni kipindi cha kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Wanafamilia watambue kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kumfuasa Kristo Yesu bila woga! Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.

Likizo ni wakati muafaka wa kutafakari kazi ya uumbaji

Likizo ni muda muafaka wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Likizo si wakati wa kumtundika Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu kwani hii, ni hatari kubwa sana! ‘Njoni ninyi peke yenu kwa faragha’ ni mwaliko wa Kristo ukitukumbusha umuhimu wa ratiba inayoweka vipengele vyote maisha katika mizania. Tuna majukumu mengi, ‘nimechelewa! nawahi! nina kazi! sina muda!’ kiasi cha kushindwa kula, kuwa na wanafamilia na marafiki au kucheza na wajukuu, mwisho tunachoka tu dunia ikiendelea kulizunguka jua na kujizungusha yenyewe kama kawaida. Daima tupo online, hatuna muda wa kufikiri na kupanga vema ndani ya vichwa vyetu, kazi ikiisha hufuata burudani,  simu kiganjani tangu tunaamka hadi tunalala usiku, na huwa tunakaribia ukichaa tunapoishiwa bando, kupoteza au kuharibikiwa simu, simu ni magaidi mifukoni, wapendwa ‘njoni, ninyi peke yenu kwa faragha.”

Likizo ni muda muafaka wa kubadilisha maisha

UFAFANUZI: Kwa kawaida tuna muda kwa mambo tunayoyapenda au yenye maslahi. Msichana humlalamikia mvulana wake kuwa hana muda naye, angependa kila dakika wawasiliane, ajue aliko na anachofanya sababu ni wa muhimu kwake. Kiuhalisia hatuna muda na mambo yasiyotuvutia. Hivi kama tunakosa muda wa kutulia, kusali, kutafakari, kukaa na familia na wenzetu maana yake mambo haya hayatuvutii ndio maana au hatuna muda nayo au tunayapa muda kidogo sana. Kristo anatuita faraghani, tumuitikie tukigeuza macho na akili zetu kutoka nje yetu na kuangalia ndani yetu, kujiona tulivyo wanyonge, masikini na wakosefu, tujifungie peke yetu na Mungu tu. na hapo tusali, tutafakari Neno, katika usikivu, bila kelele za spika au za ndimi, tutapumzika, tutayajua mapenzi ya Mungu na kuingia katika faraja yake. “Faragha” na Kristo yahusisha walau kuwa na Saa Takatifu (Hora Sancta) mbele ya Yesu wa Ekaristi ili kusali, kutafakari Neno na kuabudu. Aliiomba Mwenyewe katika saa ile ngumu akifadhaika Gethsemane “Akawajia wale wanafunzi akawakuta wamelala, akamwambia Petro, hamkuweza kukesha nami hata saa moja? Kesheni muombe msije mkaingia majaribuni” (Mt 26:40-41). Hivi kuwa faraghani pamoja na Yesu kunatufanya washiriki wa kazi ya ukombozi, kunatuwezesha kukua na kufanana naye, kunatuhamasisha kushika amri zake na kuishi ndani yake, msaada wakati wa majaribu, uhuru kutoka vifungo vya kidunia, kimwili na kiroho, kufanywa wapya tukigeuzwa kutoka ndani, kujipatia nguvu ya kimaadili inayotuwezesha kufundisha, kukemea na kuonya na kiuhalisia faragha na Kristo inatuwezesha kupambanua sauti ya Mungu na sauti ya Ibilisi.

Likizo ni muda wa: Sala, Neno la Mungu na Matendo ya huruma

‘Njoni, ninyi peke yenu kwa faragha mkapumzike kidogo…’ sio kustarehe, kulewa, kucheza, kulala hapana… ni mapumziko na Kristo, tena amesema ‘kidogo’ na hivi tusichanganye mapumziko na uvivu. Kristo anatualika kupumzika kidogo ili kupata nguvu mpya, kujijengea mizizi, kupokea neema ya msaada, kutuliza akili na moyo na kuimarisha muungano wetu na Mungu kusudi tukitoka hapo tuungane naye katika huduma sababu ‘akaona mkutano mkuu, akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji’ (Mk 6:34) Katika hili tunaalikwa kuwa wachungaji wema miongoni mwa kondoo wa Bwana. Somo la I (Yer 23:1-6) linaasa wachungaji wanaoharibu na kuwatawanya kondoo. Kwamba Bwana hatawavumilia, atainuka na kutenda Yeye mwenyewe. Basi tujitafakari namna tunavyohudumia kondoo wa Bwana yaani huduma tunayotoa kila mmoja kadiri ya sekta yake. Wazazi walee vema watoto, watoto wawatii wazazi, wafanyakazi wahudumie kwa moyo, wakulima wazalishe, huo ndio uchungaji upasao. Serikali za dunia yetu, zihakikishe ulinzi, usalama na hali njema ya raia wao, wasitunge sheria chungu na sera zinazoongeza ugumu wa maisha, walie na wananchi maisha yanapoonekana magumu na maamuzi yao pamoja na kuinua uchumi na kuongeza mapato ya nchi, yatoe nafuu kwa watu, wawatendee raia kama ambavyo angetenda Kristo Yesu Mwenyewe aliye Mtawala Mkuu wa falme, tawala na milki zote mbinguni na duniani. Tunapokuwa miguuni pa Kristo “faraghani” tukipumzika tumwambie atusaidie kusameheana, kupendana na kuvumiliana katika haki ing’arishwayo na huruma. Somo II (Efe 2:13-18) latudai umoja na mshikamano katika Kristo aliyebomoa kiambaza kilichotutenga, kuondoa uadui, kuwa wapya na kutupa amani kwa njia ya Msalaba. Shime wana wa Mungu, tupendane!

furaha ya uumbaji ni kutunza mazingira
tazama kila kitu ni chema

Similar Posts