|

Tafakari Dominika ya Huruma ya Mungu: Amani Ni Zawadi ya Kristo Yesu Mfufuka

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa maskini na wahitaji zaidi

Na Padre Joseph Herman Luwela, – Vatican. 2024-04-06
Baada ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliitangaza kuwa ni Dominika ya Huruma ya Mungu, waliosali Novena ya huruma tangu Ijumaa Kuu wanahitimisha leo. 

UTANGULIZI: Wapendwa katika Kristo mfufuka, leo tunadhimisha Dominika ya Pili ya Pasaka, tukiwa bado ndani ya kilele cha Sherehe za Pasaka (Oktava ya Paska), ni siku ya nane baada ya ufufuko Bwana wetu Yesu Kristo, na inahitimisha kipindi cha Oktava ya Pasaka. Zamani Dominika hii iliitwa Dominika nyeupe sababu waliobatizwa usiku wa Pasaka walivaa mavazi meupe siku nane, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Pasaka ikiwa ni siku ya nane waliyavaa kwa mara ya mwisho. Baada ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliitangaza kuwa ni Dominika ya Huruma ya Mungu, waliosali Novena ya huruma tangu Ijumaa Kuu wanahitimisha leo, wanapokea rehema na kufanya matendo ya huruma. Kristo alimuahidi Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kolowaska amani kwa ajili ya wakosefu wenye kujizamisha ndani ya bahari kuu ya huruma ya Moyo wake kwa ajili ya mateso ya YESU utuhurumie sisi na dunia nzima. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea.

Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari-Musoma Tanzania

UFAFANUZI: Katika Injili ya Yohane (20:19-31), tumesikia matukio mawili yanayofuatana ambapo Yesu aliyefufuka anawatokea mitume wake. Tukio la kwanza ni mara baada ya Yesu kufufuka, anawatokea mitume kumi ambao walikuwa wamejifungia ndani ya chumba, bila amani, wakijaa woga na hofu ya Wayahudi, wakiogopa kuteswa na kufa kama Bwana wao. Hapo Yesu anawatokea, anawaimarisha na kuwafariji kwa kuwapa amani ya ufufuko.  Amani kwenu! Kadiri ya Kamusi amani ni hali ya usalama isiyo na ghasia, fujo au vita, hali ya utulivu. Kidini amani ni hali njema, baada ya Mungu kumaliza kuumba “na tazama kila kitu kilikuwa chema” (Mwa 1:31) yaani kila kitu kilikuwa katika amani na uhusiano mwema na Mungu. Sentensi hii “na tazama kila kitu ni chema” iliharibiwa na malaika waovu na wazazi wetu wa kwanza, tukafukuzwa paradiso: mahali pa furaha na raha, mahali pa amani. Tukiwakilishwa na wazazi wa kwanza, tukatoka Paradiso vichwa chini, mikono nyuma, tumenyong’onyea, amani imetoweka. Mungu akatuonea huruma na kutuahidi “urafiki ule uliovunjika, amani iliyotoweka, Mimi Mungu wenu nitairudisha tena ili wanadamu muwe katika amani na Mimi Mungu wenu” (Mwa 3:15). Katika Somo la kwanza (Mdo. 4:32-35;) tumesikia jumuiya na jamii ya wakristo wa kwanza wakishuhudia ufufuko wa Bwana kwa maneno na zaidi sana kwa matendo ya upendo kwa Mungu na kwa jirani, wakiwa roho moja na moyo mmoja katika Kristo. Walikuwa wakisali, wakitafakari Neno la Mungu na kuumega Mkate (Adhimisho la Misa Takatifu). Zaidi sana walikusanya mali zao zote na kuzitumia kwa ushirika, umoja na usawa; hapakuwepo malalamiko, ufisadi, uchoyo, wivu, husuda, wala wizi. Haya ndiyo maisha ya ufufuko yanayoakisi maisha ya Mbinguni, ambayo familia, jumiya na taasisi zetu zinashindwa kuishi leo kikamilifu.

Waamini wakishiriki katika semina kuhusu huruma ya Mungu, Kiabakari, Musoma

Miaka, karne, millennia ikapita, Mungu akatimiza ahadi yake kwa njia ya Kristo aliyetukomboa na kuturudishia tena amani. Ndiyo maana Kristo anapozaliwa tangazo la kwanza kwa njia ya Malaika ni “Utukufu kwa Mungu juu, na amani duniani kwa watu aliowaridhia” (Lk 2:14). Ndilo jukumu la Kristo; kuuletea ulimwengu amani, kuurudisha urafiki na Mungu na kutupatia tena Paradiso ya milele. Maandiko matakatifu yanatuambia “Bwana Mfalme ameketi milele atawabariki watu kwa amani” (Zab 29:11) Baraka zinatolewa kwa Jina la Baba na la Mwana na Roho Mt tukiomba tujaliwe na tutembee katika amani, rej. “nendeni na amani”. Mmoja akikosewa anaposamehe husema “usijali dear, yameisha uwe na amani”. Hali ya amani inapokosekana rohoni mtu hutapatapa, anakosa kwa kushika, kuongea peke yake, kuchanganyikiwa, hana raha. Sisi tuna hitaji la amani: Amani na Muumba: Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa akili yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa roho yako yote. Amani na Jirani: Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Yale usiyotaka kutendewa usiwatendee wengine. Amani na nafsi yako mwenyewe – shinda vilema vyako – mizizi ya dhambi: Uvivu, Uchochezi, ulafi, ulevi, uchoyo, chuki, masengenyo, hasira, uzinzi na wivu. Amani katika kazi na uongozi: tenda haki utawa washeria, timiza wajibu wako kazini na utumeni, Kristo anawapa Mitume zawadi ya kwanza ya Pasaka “AMANI”na amri ya kuondolea dhambi ili tu amani ipatikane kwa njia ya huruma na msamaha, basi tuamini japo hatumuoni tukisema na Mtakatifu Thoma “Bwana wangu na Mungu wangu”.

Dominika ya Huruma ya Mungu

Amani kwenu – tuwe watu wa amani, tuidumishe katika nafsi zetu ili tuwe na afya njema, pasi hofu wala mashaka. Halafu tudumishe amani kwa pamoja kama Taifa kusudi tunu hii adhimu isipotee. Ni rahisi kupoteza amani lakini kuipata tena kati ya ghasia sio rahisi. Amani si tunu inayojitegemea bali huzaliwa ndani ya mioyo yenye utu, haki, heshima, ukweli na umoja. Na tuirejee misingi ya maendeleo yetu ambayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Amani kwenu – hii ni amani inayotishiwa na tofauti za kiuchumi, wenye nguvu wanamiliki uchumi na wanawamiliki masikini wanaoendelea kukandamizwa na kunyonywa. Haki inauzwa na mnyonge anaonewa… tutadumisha amani siasa isipoingilia weledi. Mfano kuruhusu siasa na wanasiasa kuingilia mifumo na utendaji wa afya, elimu nk sio sawa. Kila mara zinaibuka sera ambazo msingi wake ni ubunifu usiozingatia weledi na hivi kufanya huduma hizo kudidimia, hakuna unyenyekevu katika kusikiliza na kushauriana na wataalamu. Amani kwenu – amani hii itadumu tukitunza mazingira bila kuyaharibu, vyanzo vya maji, misitu, miti ya asili visiingiliwe na shughuli za kilimo, viwanda, majengo na takataka za sumu. Maeneo yakiharibika ugomvi utatawala, njaa na mifarakano kati ya wakulima na wafugaji vitaendelea. Ardhi haitakuwa na rutuba, mvua haitanyesha, joto, ukame, vifo na karaha za daima. Amani kwenu – ni maneno ya faraja kwangu na kwako. Hapohapo yanatudai jukumu la kiutendaji yaani kuupeleka na kuusambaza ujumbe huu kwa wote. Namna gani? Maneno na matendo yetu yasadifu amani itokanayo na ufufuko wa Kristo na tangazo la “amani kwenu.” Kila mmoja wetu awe mtangazaji wa ujumbe uletao amani badala ya hofu katika jamii.

Dominika ya Huruma ya Mungu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu

Wahubiri wanapowatangazia wengine amani ya Kristo, wao wenyewe waishi kwa amani na wenzao. Mfano, padre na padre mwenzake, mapadre na waamini, baba na mama, wazazi na watoto, wanafunzi na walimu, waajiri na waajiriwa, wagonjwa na wauguzi, sote kabisa na tuishi kwa amani. Mpendwa una amani na familia yako? jirani, ofisini, maisha yako ni kuvumilia tu? Ni nini kinakuondolea amani? Utakaa hali hii hadi lini? Ufarijiwe na neno la Kristo mfufuka ‘shalom aleichem!’ Amani kwenu – ni ujumbe kwa familia. Familia zitafikia kipeo cha ku mtambua Yesu kama Thomas na kukiri ‘Bwana wangu na Mungu wangu’ ikiwa wanafamilia tutaishi kwa amani, baadhi ya wazazi wamefika kuona polisi ndio msaada kwa watoto wao. Baadhi ya wanandoa hawako tayari kuvumiliana na kuchukuliana, mapato yake upendo unasinyaa, kukata tamaa kunatawala na amani inakosekana. Bado imani za kishirikina zinatutesa, tunakamatana uchawi, tunaagua, hatuna furaha, katika mazingira haya hatuwezi kuwa watu wenye amani, Mungu atuhurumie na atusaidie. Somo la Pili linakazia zaidi juu ya Upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani, kwamba kama kweli tunampenda Mungu, tutampenda Mwanae Yesu Kristo. Na kama kweli tunampenda na kumshuhudia Yesu Kristo mfufuka, tutapendana sisi kwa sisi, tuliofanywa wana wa Mungu kwa Roho Mtakatifu, kwa maji ya Ubatizo na kutakaswa kwa damu ya Kristo Msalabani iliyomwagika kwa ajili ya uzima wa roho zetu. Bikira Maria, Malkia wa mbingu atuombee sababu ulimwengu wetu una maelekeo ya kuipoteza amani aliyotuletea Kristo mfufuka – ili Mungu atujalie kuthamini na kupigania amani duniani, ili viongozi wa kanisa watetee na kupigania amani duniani hata ikiwagharimu maisha, ili viongozi wa serikali wajitahidi kutoisulubisha amani katika utumishi wao, nasi tuifurahie amani nafsini mwetu mpaka ukamilifu wa dahari. Maneno “Bwana wangu na Mungu wangu” yasikike mioyoni mwetu wakati wote. Maneno “amani kwenu” yatupe faraja na ari ya kuidhihirisha imani yetu, basi ‘Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu – roho, mioyo na miili yenu mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo’ (1Tes 5:23). Kristo amefufuka ametutakia amani na hii ndiyo Pasaka, maisha ya amani. 

Similar Posts