Waamini Walei na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushirika na Utume!

Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Fransisko, anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Umoja, upendo na mshikamano ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa.

Na Padri J0seph Herman Luwela-Kibaru wa Kristo -Vatican -Roma

yama na Mashirika mbalimbali ya Kitume yaliyoibuka baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Vyama na mashirika haya yanapaswa kupokelewa kwa imani na moyo wa shukrani, kama rasilimali kwa Kanisa, ili hatimaye, viweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha yao. Ikumbukwe kwamba, vyama vya kitume ni kama shule ya imani, matumaini na mapendo. Hapa ni mahali ambapo waamini wanaweza kusaidiana katika: imani, maisha ya kisakramenti, maadili na sala. Karama ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa waamini ndani ya Kanisa, tukio ambalo ni endelevu linalowapatia changamoto wahusika, kuzitumia karama hizi kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa kadiri ya busara na hekima ya viongozi wa Kanisa. Vyama na mashirika ya kitume yanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, waamini walei wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Kanisa la Kristo kwa kushirikiana na wakleri pamoja na watawa. Vyama na Mashirika mbalimbali ya kitume, yajenge na kudumisha utamaduni wa kushika sheria, kanuni na miongozo inyotolewa na Maaskofu mahalia, ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano kama sehemu ya muhimu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ikumbukwe kwamba, ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo huanzia ndani ya familia, jumuiya ndogo ndogo za kikristo, vigango, parokia, jimbo na Kanisa katika ujumla wake. Ikiwa kama vyama vya kitume vitashindwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, Kanisa linaweza kujikuta likiogelea katika kinzani na migogoro isiyokuwa na tija hata kidogo!

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika toba, wongofu na unyenyekevu

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na wongofu wa kimisionari na shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuzaa matunda yanayokusudia sanjari na kupyaisha sera na mikakati ya shughuli za kimisionari ndani ya Kanisa. Waamini walei ndani ya Kanisa wanapaswa kutambua dhamana na wajibu wao kama wabatizwa, yaani watu waliozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu; wanao wajibu na haki zao msingi zinazopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kimsingi waamini walei wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Mfufuka mintarafu uhalisia wa maisha yao. Waamini walei daima wajibidiishe kuchota utajiri na amana ya maisha yao ya Kikristo kutoka katika: Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa, dira na mwongozo wa jinsi ya kuyatakatifuza malimwengu. Waswahili wanasema, “kitu kizuri na chema, kula na ndugu yako.” Waamini walei watambue kwamba, amana na utajiri huu wanapaswa kuwashirikisha pia jirani zao kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; katika kuyatakatifuza maeneo ya kazi pamoja na utume wa familia. Waamini walei wakiwa wamepyaishwa kutoka katika undani wa maisha yao, wanaweza sasa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu; watu wenye wenye uwezo wa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio cha Dunia Mama kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kilio cha maskini wanaowazunguka; watu wanaoweza kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi; ukarimu na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini walei dumisheni: umoja, upendo na mshikamano.

Upya wa maisha unawataka waamini walei kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya dhati na viongozi wa Kanisa, ili kuwajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa, kila mwamini akijitahidi kutekeleza wajibu wake. Kuna kishawishi kikubwa miongoni mwa waamini walei cha kudhani kwamba, wanaweza kufanya yote kwa nguvu na jeuri yao, kwa kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele, sera na mikakati ya maisha yao. Katika mtindo na mwelekeo kama huu, vi vigumu sana kuweza kutekeleza ndoto ya Mungu katika maisha yao. Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji maparokiani na majimboni. Kwa njia hii, waamini walei wataweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Kishawishi kingine ni kile cha kuendelea kubaki wakiwa wanaelea katika ombwe, bila kuzama na kumwilisha maana ya Kanisa la Kisinodi na umuhimu wa malezi na makuzi ya awali na endelevu kwa waamini walei. Utakatifu wa maisha ni ushuhuda wenye mvuto katika maisha na utume wa Kanisa. Changamoto, matatizo na fursa mbalimbali zinazoendelea kuibuliwa ndani na nje ya Kanisa, ni mahali muafaka ambapo waamini walei wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Waamini walei wasikatishwe tamaa na dhuluma, nyanyaso na magumu wanayokabiliana nayo katika maisha na utume wao hapa duniani, bali waendelee kusimama kidete kama mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Huruma na upendo wa Mungu uwaimarishe na kuwapyaisha kutoka katika undani wa maisha yao!

Ustawi, maendeleo na mafanikio ya Kanisa yanapata chimbuko lake kwenye familia

i katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, hivi karibuni liliandaa mkutano wa waratibu wakuu wa Vyama na Mashirika ya Kitume, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Changamoto ya Sinodi kwa Ajili ya Utume.” Mama Kanisa kwa njia ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi anapita katika kipindi cha majadiliano, tafakari na mashauriano ili kuweza kutekeleza kikamilifu mwelekeo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ambayo ni sehemu ya asili yake kama Fumbo la ushirika kwa mfano wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni mkutano ambao umepembua kwa kina na mapana ushiriki wa waamini katika imani ndani ya vyama na mashirika ya kitume, kwa kukazia ushiriki wa waamini walei katika muktadha wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji yam tu mzima kiroho na kimwili; umwilishaji wa Injili ya upendo katika uhalisia wa maisha ya watu pamoja na utekelezaji wa shughuli za kijamii. Washiriki wa mkutano huu wameangalia kwa kina na mapana vipimo mbalimbali vya Sinodi vinavyoleta changamoto mpya kwa ukuaji wa vyama na mashirika haya ya kitume. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu dhana ya Sinodi kwa watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.” Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Kardinali Kevin J. Farreli: Umoja, ushirika na utume.

Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Utekelezaji wa dhana hii ni mwaliko wa kuondokana na ubinafsi na kuanza kujikita katika fadhila ya unyenyekevu, kwa kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu na maongozi ya Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini walei kushinda kishawishi cha kutaka kujifungia katika ubinafsi wao, woga na uchoyo. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni mwaliko wa kuvunjilia mbali changamoto hizi na kuanza kujikita katika mtazamo mpya wa utekelezaji wa shughuli za kichungaji, kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa watu wa Mungu, tayari kujikita katika fadhila ya unyenyekevu, wongofu wa maisha ya kiroho yanayofumbata upendo wa Mungu. Umoja na ushirika wa watu wote wa Mungu ni jambo la msingi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Vyama vya kitume na mashirika ni kwa ajili ya ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na wala si kwa ajili ya mafao ya watu wachache ndani ya Kanisa. Ni mwaliko wa kutumia karama na mapaji ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa katika ujumla wake. Huu ni mwaliko kwa wabatizwa wote.

yama na mashirika ya kitume ni kwa ajili ya utume wa Kanisa

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha amekazia umuhimu kwa waamini walei kujikita katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kujikita katika: Amri za Mungu pamoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Leo hii, kuna vyama na mashirika ya kitume yapatayo 117 ambayo yako chini ya usimamizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi si kugawana madaraka na waamini walei, bali huu ni mchakato wa ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika umoja, ushirika na utume, kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko kwa mapadre na waamini walei kutembea kwa pamoja chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu tayari kushiriki kikamilifu maisha na utume wa Kanisa.


Similar Posts