Wosia wa Kiroho wa Papa Fransisko Na Uthibitisho wa Kifo Chake

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa maisha ya kiroho, aliouandika tarehe 29 Juni 2022, kwanza kabisa alijikabidhi kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu

Hayati Papa Francisko anasema siku zote amekabidhi maisha na huduma yake ya Kipadre na Kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Bwana wetu Kristo Yesu, Bikira Maria Mtakatifu. Anaomba kwamba, maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika, katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, huku akingojea Siku ya ufufuo wa wafu. Alitamani kuona safari yake ya mwisho ya hapa duniani iishie mahali patakatifu pa Bikira Maria, mahali ambapo alienda kusali.

Na Pd. Joseph Luwela-Vatican Roma-Italia

Mazishi ya Baba Mtakatifu yanatarajiwa kufanyika Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali. Kuanzia Jumatano tarehe 23 Aprili 2025 Mwili wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko utawekwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuwawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa heshima zao za mwisho.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Papa Francisko   (ANSA)

Nembo ya Kiaskofu: “Akamwangalia kwa huruma, akamchagua” “Miserando atque eligendo” ni maneno ya kauli mbiu ya yaliko kwenye Nembo la Kiaskofu ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kama kumbukumbu endelevu ya maisha ya wito wake alipokuwa kijana, pale Mwenyezi Mungu alipomwangalia kwa huruma na kumchagua. Shughuli za kichungaji kuhusu miito ni mchakato wa kukutana na Kristo Yesu, tayari kumchagua na kumwambata katika maisha. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa maisha ya kiroho, aliouandika tarehe 29 Juni 2022, kwanza kabisa alijikabidhi kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anasema, kwa kuhisi kwamba, mwisho wa maisha yake ya hapa dunia unakaribia na akiwa na tumaini hai katika uzima wa milele, alipenda kuelezea mapenzi yake kuhusu mahali pa kuzikwa kwake.

Papa Francisko katika wosia wake: Azikwe Kanisa kuu la B.Maria Mkuu  

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema siku zote amekabidhi maisha na huduma yake ya Kipadre na Kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Bwana wetu Kristo Yesu, Bikira Maria Mtakatifu. Anaomba kwamba, maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika, katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, huku akingojea Siku ya ufufuo wa wafu. Alitamani kuona safari yake ya mwisho ya hapa duniani iishie mahali patakatifu pa Bikira Maria, mahali ambapo alienda kwa ajili ya sala mwanzoni na mwishoni mwa kila hija ya kitume, ili kukabidhi nia yake kwa Bikira Maria pamoja na kumshukuru kwa unyenyekevu, ulinzi na tunza yake ya kimama. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anaomba kaburi lake liwekwe kwenye Kikanisa cha Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani.”

Watu wameanza kutoa heshima zao za mwisho kwa Papa Fransisko

Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitaka kaburi lake lichimbwe ardhini, rahisi bila mapambo maalum bali libaki likiwa na maandishi ya pekee “Franciscus.” Gharama ya maandalizi na hatimaye maziko yake, zitagharimiwa na mfadhili ambaye amempanga, safari ya kuhamishiwa kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tayari alitoa maagizo kwa Kardinali Rolandas Makrikas, Kamishna Maalum wa Kipapa wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Hayati Baba Mtakatifu anawaombea thawabu stahiki kwa Mwenyezi Mungu wale wote waliompenda na watakaoendelea kumwombea. Anasema, alitolea mateso aliyokumbana nayo katika sehemu ya mwisho wa maisha yake kwa Bwana kwa ajili ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kati ya watu!

Papa Francisko Kuzikwa Kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu, Roma

Tarehe 21 Aprili 2025 Profesa Andrea Arcangeli, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican alitangaza rasmi kwamba, Baba Mtakatifu Francisko “Jorge Mario Bergoglio aliyezaliwa tarehe 17 Desemba 1936 aliyekuwa anaishi mjini Vatican na Mwenyeji wa Vatican amefariki dunia saa 1:35 Asubuhi ya tarehe 21 Aprili 2025 katika chumba chake cha “Domus Santa Marta” Hosteli ya Mtakatifu Martha kutokana na ugonjwa wa: “Kiharusi, Kwa kupoteza fahamu, Koma pamoja na Ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu. Baba Mtakatifu pia alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa: Mkamba, Kisukari pamoja na Shinikizo la damu. Uamuzi wa kifo hiki umeamriwa na rekodi iliyotolewa na chombo kinachojulikana kama “electrocardiothanatographic” akatangaza kwamba, sababu za kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kulingana na ufahamu wake na dhamiri nyofu ni hizo zilizotangwa hapo juu anasema Profesa Andrea Arcangeli, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican.

Similar Posts