Jumatano ya Majivu: Katekesi Kuhusu Kipindi cha Kwaresima.
Kipindi cha Kwaresima ni fursa ya kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wainjilishaji wote, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kile wanacho amini, kufundisha na kuadhimisha. Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na utakatifu.
Na Padre Paschal Ighondo, – Vatican.Italia
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumatano ya Majivu. Ni siku ya kwanza ya kipindi cha Kwaresma mwaka B, 2024, katika Liturujia ya Kanisa. Ujumbe wa Kwaresima Baba Mtakatifu Fransisko mwaka huu 2024, umejikita katika maneno haya; “Kupitia jangwa, Mungu anatuongoza kwenye wokovu” (Kut. 20:2). Tafakari hii nimependelea iwe kama Katekesi inayohusu thamani ya maadhimisho ya matukio mbalimbali katika historia ya wokovu wetu. Ndiyo maana kabla ya kuyatafakari masomo ya siku hii ya Jumatano ya majivu, ni vyema kujikumbusha baadhi ya mambo muhimu katika siku hii na kwa kipindi hiki cha Kwaresima. Kipindi cha Kwaresima ni fursa ya kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wainjilishaji wote, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kile wanacho amini, kufundisha na kuadhimisha. Iwe ni fursa ya kugundua na kutambua kwamba, wao kama waamini ni Mitume wa Yesu, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji.
Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kwanza kabisa, tukumbuke kuwa Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za vita vya kiroho. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo katika maadhimisho ya siku hii anatuombea akisema; “Ee Bwana, utujalie sisi waamini wako tuanze vita vya roho kwa mfungo mtakatifu. Nasi tulio tayari kupigana na pepo wachafu tujipatie nguvu kwa sababu ya kufunga”. Silaha za vita hivi ni sala na mfungo unaojikita katika kulisoma na kutafakari Neno la Mungu, na kufanya matendo ya huruma kwa bidii zaidi tukiongozwa wa amri kuu ya mapendo. Ni kipindi cha kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo.
Pili, Kwaresima ni kipindi cha toba, kipindi cha kujipatanisha na Mungu, kujipatanisha na Kanisa, kujipatanisha na ndugu, jamaa na marafiki na kujipatanisha mtu na nafsi yake, kujisamehe na kuwasamehe wengine maana hata sisi Mungu anatusamehe tunapoomba msamaha na kufanya toba ya kweli kama wimbo wa mwanzo unavyooimba ukisema; “Ee Bwana, wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba. Unawasamehe watu dhambi zao kwa ajili ya kufanya kitubio na kuwahurumia kwa kuwa ndiwe Bwana Mungu wetu” (Hek. 11:24-25, 27). Tatu, Kwaresima ni safari ya hija ya kiroho ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu – mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo – Pasaka. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya kubariki majivu tunayopakwa kama alama na ishara ya kukubali kuwa tu wadhambi wanaofanya toba anasali kwa ajili yetu akisema; “Ee Mungu, unayependezwa na unyenyekevu na kutulizwa na kitubio chetu, usikilize kwa wema sala zetu. Uwashushie kwa rehema baraka yako watumishi wako watakaopakwa majivu haya; ili baada ya kutimiza wajibu wa Kwaresima waje waliadhimishe fumbo la Pasaka la Mwanao, wakiwa wametakata rohoni”. Na katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisema; “Ee Bwana, tunatoa sadaka hii ya kuanzia Kwaresima, na kukuomba tuzishinde tamaa mbaya kwa matendo ya kitubio na mapendo. Nasi tukisha takaswa dhambi, tuwe na ibada ya kuadhimisha mateso yake Mwanao.” Kumbe, kusali, kufunga, kutenda matendo ya huruma kwa upendo, kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu, ndizo nguzo kuu msingi za kipindi hiki cha Kwaresima.
Jambo la nne ni tahadhani. Kuna uwezekano wa kufikiri na kudhani kuwa hakuna jipya katika kipindi cha Kwaresima cha mwaka huu na cha mwaka uliopita. Tukumbuke kuwa kila adhimisho la tukio lolote la kiliturujia katika historia ya wokovu wetu linapoadhimishwa katika mzunguko wa mwaka wa kiliturujia, lina hali mbili. Kwanza ni kutukumbusha yaliyotokea zamani katika historia ya ukombozi wetu. Na pili ni kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho. Kumbe maadhimisho haya ya kiliturujia yanafanya sehemu ya maisha yetu na yanatufanya tuonje upendo wa Mungu katika mafumbo yanayoadhimishwa katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani tunapoelekea katika maisha ya umilele mbinguni. Kwa minajili hii, kila mwaka wa kiliturujia ni mpya na wa pekee. Hakuna mwaka unaofanana na mwingine. Maana kila mwaka unapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na hivyo kutuleta karibu zaidi kwa Mungu. Kumbe tusikianze kipindi hiki kwa mazoea kana kwamba hakuna jipya lolote. Bali kwa unyenyekevu na usikivu mkuu, tufungue macho na masikio ya mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi hiki kitakatifu.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yoeli (2:12-18). Katika somo hili Mungu kwa kinywa cha Nabii Yoeli anatuita tumrudie Yeye kwa mioyo yetu yote, kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza. Tunaambiwa tuirarue mioyo yetu, na siyo mavazi yetu. Katika siku za Agano la Kale, watu walikuwa na desturi ya kurarua mavazi yao kama ishara ya kufanya toba. Hata hivyo, walikuwepo wengine walioyararua mavazi yao kama ishara tu ya nje. Lakini ndani ya mioyo yao hawakuwa na toba ya kweli. Mioyo yao ya “jiwe” haikubadilika, walibaki kama walivyokuwa tangu awali. Tunaalikwa tusifanye hivyo. Tuwe na toba ya kweli. Nabii Yoeli, anatuita tumrudie Mungu kama mtu mmoja mmoja na pia kwa jumuiya. Maana kuna dhambi na makosa ya mtu mmoja mmoja na kuna dhambi na makosa ya jumuiya au jamii. Kumbe huu ni mwaliko na wito wa toba kwa watu wote; wazee, vijana na watoto. Ni mwaliko wetu sote kufanya toba ya kweli na kumrudia Mungu. Ni katika muktadha huu, siku ya kwanza ya Kwaresima inapambwa na tendo la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso. Tendo hili ni ishara ya kukubali kuwa tu wa dhambi tunahitaji kufanya toba ili tusamehewe. Ndiyo maana katika wimbo wa katikati tunaimba na mzaburi kwa matumaini makubwa tukiitegemea huruma ya Mungu tukisema; Uturehemu, ee Bwana, kwa kuwa tumetenda dhambi. Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu, na dhambi yangu i mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, na kufanya maovu mbele za macho yako. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso wako, wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; unitengemeze kwa roho ya wepesi. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, na kinywa changu kitazinena sifa zako (Zab. 51:1-4, 10-12, 15). Basi, wimbo huu iwe sala yetu tunapoanza kipindi hiki kitakatifu.
Somo la pili ni la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2Kor 5:20-6:2). Katika somo hili Mtume Paulo anatusihi tupatanishwe na Mungu kwa njia ya Kristo Mwana pekee wa Mungu ambaye Mungu mwenyewe alimtuma aje kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Mungu asiyejua dhambi alimfanya Yesu kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (2Kor 5:21). Yesu Kristo hakujua dhambi, lakini alifanywa kuwa dhambi ili sisi tusio haki tufanywe kuwa haki katika Yeye. Sisi wadhambi tulistahili adhabu ya kifo. Lakini Kristo aliteseka na kufa ili sisi tusamehewe dhambi zetu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 6:1-6;16-18). Katika Injili hii tunapata mafundisho ya Yesu ya namna tunavyopaswa kukiishi kipindi hiki cha Kwaresma. Yesu anatuonya tusiwe wanafiki, tusifanye matendo mema ili tuonekane machoni pa watu wengine. Maana tukifanya hivyo tunakuwa tumepokea thawabu yetu kwa njia ya watu wanaotutazama, kutustaajabia, na kutusifia. Kumbe, matendo yetu mema yasilenge kujionesha kwa watu. Bali yawe ni mawasiliano binafsi kati yetu na Mungu, yaani kujenga muungano na Mungu wetu aliyemtakatifu kwa sala, sadaka, kufunga na matendo ya huruma kwa upendo. Hivyo basi, ili tuweze kukiishi vyema kipindi hiki cha kwaresima na kupata matunda yake, hatuna budi kutenga muda wa sala, kufanya toba na malipizi, kujikatalia furaha za kimwili, kuwasaidia na kuwatendea kwa ukarimu na upendo watu walio wahitaji. Matendo haya ni dawa za kutuponya na ugonjwa wa ukiro – ukosefu wa kinga ya rohoni, dhambi.
Basi na tukiingie kipindi hiki kama vile ni cha kwanza na cha mwisho katika maisha yetu. Tuitumie vyema kwaresma hii kana kwamba hakuna tena Kwaresma nyingine. Mtume Huu ni ndio wakati uliokubalika, siku ya wokovu ndiyo sasa. Tusisubiri wakati mwingine. Tumwombe Mwenyezi Mungu, ili kwa neema zake, kwaresima hii itusaidie tutekeleze mapenzi yake Mungu kwa kuzaa matunda mema kwa wakati wake kama antifona ya wimbo wa Komunio inavyotuambia; “Mwenye kuitafakari sheria ya Bwana mchana na usiku, atazaa matunda yake kwa majira yake” (Zab. 1:2-3). Na Sala baada ya Komunyo inahitimisha ikisema; “Ee Bwana, Sakramenti tulizopokea zituletee shime yako, ili kufunga kwetu kukupendeze, kutupatie nasi dawa ya kutuponya”. Nawatakieni mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima. Tumsifu Yesu Kristo!