|

Ufufuko wa Yesu ni Kilele cha Ukweli wa Imani Katika Kristo Yesu

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli.  (SumbawangaMedia)

Na. Padre Joseph Herman Luwela-Kutoka Vatican Rome

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli

UTANGULIZI:Mpendwa msikilizaji na msomaji, wa tafakari zetu ile siku tuliyoisubiri kwa hamu kubwa tena kwa siku 40 toka Jumatano ya Majivu; imewadia. Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Kaburi tupu na vitambaa vilivyolala ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka. Kristo Yesu wa kwanza katika wafu ni msingi wa ufufuko wetu, tangu sasa kwa kufanywa haki roho yetu na baadaye kwa kuhuishwa miili yetu. Rej. KKK 638-658. Ni Pasaka, sherehe ya UFUFUKO WA BWANA, sherehe kubwa kuliko zote katika Kanisa Katoliki. Kristo amefufuka, Kristo kweli kweli ameshinda mauti. Wapendwa wana wa ufufuko, katika somo la Injili, Mwinjili Yohane ametupatia ushuhuda wa kimazingira uliomfanya yeye mwenyewe aamini kuwa Bwana wake Yesu kweli amefufuka, na anatutaka nasi tuamini kuwa Bwana kweli amefufuka, ili tuweze kuupuuza uzushi wowote ule wa watu wanaosema kuwa Yesu hakufufuka bali wanafunzi wake waliuiba mwili wake na kisha wakaanza kushuhudia kuwa amefufuka. Ushuhuda wa kwanza wa kimazingira wa ufufuko wa Yesu ni kaburi kuwa wazi.

Kaburi wazi ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka

Tukumbuke kuwa Bwana Yesu Kristo alipozikwa liliwekwa jiwe kubwa kabisa pale penye mlango wa kaburi lake. Jiwe hilo liligongwa muhuri, na waliwekwa pia walinzi ili walilinde kaburi lake. Kwa hiyo, kutokana na maelezo hayo isingekuwa rahisi kwa mtu au watu kulisukuma jiwe hilo na kuuiba mwili wake kama wengine wanavyodai. Ushuhuda wa pili wa kimazingira ni wa vitambaa (sanda) na leso (ambayo tumesikia kuwa haikuzongwazongwa na vitambaa bali ililala mahali pa peke yake) ambavyo vilivyokutwa kaburini. kama mwili wa Yesu ungekuwa umeibiwa, hakika wezi hao ama wangeuchukua mwili pamoja na sanda yake au kama wangeifungua sanda na leso vingekuwa vimerushwarushwa huko na kule kwa sababu ya haraka ili wasikamatwe. Lakini mwinjili Yohane ametueleza kuwa vitambaa na leso vilikutwa vimelala namna ile ile kama walivyokuwa wamemzika. Huu ulikuwa ni ushahidi wa uhakika kuwa Bwana amefufuka kwani mara baada ya kuona vitambaa na leso vilivyolala namna ileile kama mwili upo, Mtume Yahane aliaminiNawaalikeni, tutafakari ujumbe huu wa leo “wamemwondoa Bwana na hatujui walikomweka.”

Pasaka ni fumbo letu la wokovu.

UFAFANUZI: Sherehe ya Pasaka ilikuwa ikisherehekewa hata kabla ya kuja Kristo. Ilikuwa ni sherehe ambayo wayahudi walikumbuka kule kukombolewa kwao na Mwenyezi Mungu toka utumwani Misri, toka mikononi mwa Farao. Waliyakumbuka matendo makubwa ya Mungu, wakati harakati za kuwarudisha tena katika nchi ya Ahadi. Katika somo la kwanza tumesikia jinsi Mtume Petro akiwa pamoja na mitume wenzake wanashuhudia kwa ujasiri ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Wale ambao hapo awali walikuwa wamekata tamaa na kujawa na hofu kutokana na yale matukio yaliyotukia siku ya Ijumaa Kuu yaani mateso na kifo cha aibu cha Bwana wao pale msalabani, sasa tukio la ufufuko wa Yesu linawabadilisha kutoka katika hali ya kukata tamaa na kujawa na hofu, sasa wanajawa matumaini mapya, nguvu na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia waziwazi kuwa Bwana kweli amefufuka. Wayahudi baada ya kumwua Yesu, walimzika mapema ili waweze kufurahia “Pasaka yao ya kawaida”. Lakini kwa mitume na wafuasi wa Yesu, kwao ilikuwa ni tukio lililowakatisha tamaa. Desturi ya Kiyahudi ilikuwa ni kwenda kupaka mafuta maiti kwa Muda wa siku tatu. Kwa bahati mbaya wafuasi wa Yesu hawakwenda siku ya pili kwani ilikuwa ni sabato. Walilazimika kwenda siku ya tatu. Nao ni Akina mama Maria Magdalena na yule Maria Mwingine. Cha ajabu walipofika huko wakakuta mwili wa Yesu haupo. Hofu ikawashika, lakini kwa vile hawakuwa na mamlaka ya kushuhudia tukio kama hilo; wakapasika kurudi kwa wanaume, yaani mitume kuwapasha habari hii kwa ujumbe mzito huu “WAMEMWONDOA BWANA KABURINI, NA HATUJUI WALIKOMWEKA”. Hapa tunaona jinsi nafasi ya mwanamke katika jamii inayorudishwa na Kristo mfufuka wanakuwa wakwanza kushuhudia na kutoa habari za ufufuko wa Kristo.

Pasaka ya Bwana iwajengee watu imani, matumaini na mapendo

Maneno haya ya Maria Magdalena yatutafakarishe kidogo. Mosi, kwa nini alikwenda kaburini tena alfajiri? Na je, aliona nini kuthibitisha kuwa mwili wa Yesu haukuwemo mle Kaburini? Tena, kwa nini alidhani kuwa ule mwili umeondolewa na watu fulani? Maria Magdalena alikuwa ni mtu mwenye historia ya dhambi nyingi hapo kabla. Yeye alipata bahati ya kusamehewa dhambi zake na Yesu. Alipendwa na Yesu, naye akajibu upendo huo kwa Kumpenda Yesu kama Mwokozi. Na hata baada ya kifo bado upendo wake kwa Yesu haukukauka. Kwa bahati mbaya inaonesha hakuwa na habari yoyote juu ya Ufufuko. Kuondolewa kwa jiwe ambalo lilitumika kufunika kaburi kulikuwa ni ishara tosha kuwa maiti iliyokuwemo mle ndani haipo tena. Je, ili kufufuka Kristo alihitaji jiwe liondoke? Jiwe lile liliondolewa si kurahisisha kufufuka kwa Yesu bali ili kuwa ni alama ya kwanza ya ushahidi kwamba Yesu amefufuka. Lingeendelea kuwepo pale lilipokuwepo isingekuwa rahisi kutoa habari kirahisi nini kimetokea huko ndani ya Kaburi. Maria Magdalena alikutana na kioja hiki cha jiwe kutokuwepo mahala alipotarajia. Akashikwa na butwaa. Alihisi kuna watu wamemwondoa Yesu toka mahala pale. Je, ni akina nani? Kwa kipindi kile kuna watu walikuwa wanakwenda makaburini kuiba miili ya marehemu kwa shughuli za kishirikina. Hivi Maria Magdalena alidhani huenda kufuru hii ndio imekwenda kufanywa juu ya mwili wa Yesu. Hofu ya Maria Magdalena ilikuwa pia huenda wale wakuu wa makuhani na Mafarisayo wameutoa mwili wa Yesu wamekwenda kuuchapa bakora tena kwa vile hawakuridhika na adhabu walizompa na isitoshe Yesu alikufa mapema mno pale Msalabani. Ndugu zangu katika Kristo mfufuka, Kufika kwa mitume wale wawili Petro na Yohane ndiko kunaanza kutoa rasmi taarifa ya kufufuka kwa Yesu. Hadi leo, hakuna aliyeandika chochote iwe ni kwenye Biblia au kwenye Vitabu vinginevyo ni namna gani Yesu alifufuka. Kwa kifupi hakuna aliyeshuhudia tukio hilo. Yaliyoandikwa kuhusiana na ufufuko wa Yesu ni matukio baada ya tukio la Yesu kufufuka, mfano, kaburi kuwa wazi, sanda na vitambaa vingine kuwepo kaburini, Yesu kuwatokea wanafunzi na wafuasi wake sehemu mbalimbali. Yote haya yanatuthibitishia kuwa Kristo alifufuka. Hivyo, hakuondolewa kama alivyodai Maria Magdalena. Bali alifufuka, alikuwa hai

Pasaka ya Bwana iwajengee watu imani, matumaini na mapendo

Katika Somo la Pili (1 Kor. 5: 6-8) akiwaandikia Wakristo wa Kanisa la Korintho anawaonya kwa kuwaambia kuwa, “Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo, basi na tufanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.”  Ujumbe huu ambao mtume Paulo anautoa kwa Wakorintho wa kuishi maisha mapya na kuachana na ukale yaani maisha ya giza (dhambi), unatuhusu nasi leo tunaosherehekea ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ujumbe huu unatutaka tufanye mabadiliko ya kweli yaani tuachane na mazoea mabaya ambayo yanatufanya tuishi gizani (dhambini), na tuishi maisha mapya yaani tutembee katika nuru inayoletwa na Kristo Mfufuka kwa kutenda mambo yaliyo mema katika maisha yetu ya kila siku. Ufufuko wa Yesu ni kilele cha safari yake ya Ukombozi wa binadamu, ni kilele cha upendo wa kimungu kwetu sisi. Ni mwaliko kwetu kuwa nasi tusibaki kaburini, bali tufufuke yaani tuwe wapya katika nafsi na mahusiano. Kila mmoja ajiulize moyoni mwake leo, ni mambo gani ambayo anataka Kristo mfufuka ayabadilishe. Je, ni tabia yangu mbaya kama vile: uvivu katika kushiriki kazi za mikono, au kusoma kwa bidii, utoro wakutohudhuria shule au uvivu katika kufika kusali Kanisani? Je, ni tabia yangu ya uchoyo, uongo, matusi, ugomvi, ulevi, wizi, uchochezi na usengenyaji, dharau na kukosa adabu kwa wazazi na walezi wetu uchu wa Madaraka, rushwa, ubinyaji wa haki za wengine n.k.  Kila mmoja wetu anajua ni mambo gani hasa anayo, ambayo yanaweza kumfanya asiishi maisha mapya ya ufufuko. Hayo mwombe Kristo mfufuka akusaidie kuyaondo na kukufanya uwe mpya kiroho na kimwili.

Fumbo la Pasaka ni muhtasari wa imani, matumaini na mapendo

Wakati wote wa kipindi cha Kwaresima tulialikwa kuzika tabia zetu mbovu na vilema vingine. Pasaka ndio wakati muafaka wa kudhihirisha kuwa sisi tu watu wa ufufuko. Si tu watu ambao tulienda likizo ya kutenda dhambi na sasa tunarudia tena hali yetu ya zamani. Hapana, sisi sasa ni watu wapya. Tuliingia katika mazoezi makubwa ya kiroho, yale mema tuliyoyapata kipindi chote cha Kwaresma mfano toba ya kweli, ukarimu kwa wahitaji na juhudi ya sala, sasa tunatakiwa kuviendeleza na viwe sehemu ya maisha yetu. Bila shaka wapo ambao hawataelewa kwa nini sisi tumebadilika. Watajaribu kututafuta katika uzamani wetu. Watajiuliza mbona umemwondoa Bwana uliyemtumikia zamani, na hata hawajui ulikomweka. Hao wote wape jibu moja tu, umebadilika, upo kipasaka zaidi. Ndugu zangu, tusisherehekee Pasaka kama ratiba tu bali kama sehemu ya sisi kukua kiroho. Tumshukuru Mungu kwamba tumepata fursa hii nasi mwaka huu. Je, watu watatutambuaje? Nasi, tulio wana wa ufufuko tuondoe mawe yanayotufanya tushindwe kudhihirisha ufufuko huo wa Yesu. Wengine tuna mawe ya fitina, chuki, ulevi, ulafi, uongo, majungu, “michepuko”, rushwa, kiburi n.k. yote hayo tuyaondoe ili Kristo mfufuka aweze kudhihirishwa kwa Maisha yetu. Leo vilevile, tuwapeleke wenzetu furaha ya Kristo mfufuka ambao kwa sababu ya ugonjwa na matatizo mengine wameshindwa kuunganika nasi. Twende pia kwa watu wote tukawaambie Bwana amefufuka, amka wewe uliyelala usingizini na Kristo atakuangaza! Kiujumla tuwe waangalifu katika kila kitu tukifanyacho ili tusije tukauzimisha mwanga wa Kristo mfufuka katika maisha yetu. Tukifanya hivyo hakika, Ufufuko wa Kristo utaleta mabadiliko chanya katika maisha yetu! Tumwombe Kristo mfufuka atujalie neema na Baraka zake katika maisha yetu ili tuweze kuishi vema maisha haya kama wana wa ufufuko na tupate kustahili kufufuliwa naye siku ya mwisho.

Similar Posts