|

Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari ya Kuwa Mama wa Mungu

Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu kwa mwaka 2024 inaadhimishwa Jumatatu tarehe 8 Aprili 2024, baada ya tarehe 25 Machi 2024 kuangukia kwenye Juma Kuu. Tarehe 8 Aprili 2024 Mama Kanisa sehemu mbalimbali za dunia anaadhimisha Siku ya Kutetea Uhai na Utakatifu wa Maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Injili ya Uhai!

Na. Padre Joseph Luwela-Vatican ROMA ITALIA
Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu kwa mwaka 2024 inaadhimishwa Jumatatu tarehe 8 Aprili 2024. 

Miezi tisa kabla ya Sherehe ya Noeli ya Bwana, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Hapa Mwenyezi Mungu anakutana na binadamu katika tumbo la Bikira Maria, bustani iliyopambwa sana na hiki ni kisima. Bikira Maria akalipokea Neno la Mungu na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu atende kazi yake na kivuli chake kikamfunika na kwa sababu hiyo kile kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Rej. Lk 1:35.; Kut 40: 34-35. Neno wa Mungu akamwilishwa tumboni mwa Bikira Maria, kwa ajili ya Kristo Yesu Mtu mpya, Mwana wa Mungu aliye hai. Kumbe Roho Mtakatifu alimwandalia makao Neno wa Mungu ili kuyafanya mapenzi ya Mungu. Rej. Ebr 10: 5.7. Jibu la Bikira lilikuwa, “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana.” Malaika Gabrieli akamjuza pia matendo makuu ya Mungu aliyomtendea binamu yake Elizabeti, kiasi cha kutoka kwa haraka kwenda kumtembelea na huo ukawa ni ufunuo wa siri kubwa iliyokuwa imefichika mjini Nazareti, tukio la kiimani, akajiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu ili kumwezesha kuandika historia ya ukombozi kwa kukubali wito wa Mungu. Sherehe hii kwa mwaka 2024 inaadhimishwa tarehe 8 Aprili 2024, baada ya tarehe 25 Machi 2024 kuangukia kwenye Juma Kuu. Bikira Maria akawa ni chombo cha imani kwa sababu aliamini kile alichoambiwa na Bwana. Elizabeti akamwona Bikira Maria kuwa kweli ni Mama wa Mungu, kwa sababu alikua amejaa neema “Fide plena.” Kwa mwitikio huo, Neno, Mwana wa Mungu na Mwana wa Adamu akafanyika mtu na hivyo Bikira Maria kubahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu. Rej. Lk 1: 38. Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele, amekuja kuyatimiza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Rej. Ebr 8-9.

Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari kuwa atakuwa Mama wa Mungu

Tarehe 8 Aprili 2024 Mama Kanisa sehemu mbalimbali za dunia anaadhimisha Siku ya Kutetea Uhai na Utakatifu wa Maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni ujumbe makini unaonesha kwamba, maisha ni matakatifu na kila mtu anayo haki ya kuishi. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watetezi wa Injili ya uhai kwa ajili ya maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo!

Waamini wengi wana ibada kwa Bikira Maria

Mwanzoni, Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, “Theotokos” ilikuwa ikijumuishwa kwenye Sherehe za kipindi cha Noeli, lakini kuanzia Karne VII, ikatengewa siku yake maalum, yaani miezi tisa kabla ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari na Malaika kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa maisha na utume wa Bikira Maria kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kujenga jamii inayosimikwa katika msingi wa haki, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Bikira Maria yuko mbinguni anaendelea kusali na kuwaombea waamini wote! Bikira Maria anasali hasa zaidi kwa wale wasiosali, kwa sababu ni mama wa wote. Waamini wanahimizwa kuwa ni vyombo, mashuhuda wa upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Kanisa anamkumbuka Bikira Maria aliyepokea mpango wa Mungu katika maisha yake kwa unyenyekevu na utashi mkuu, ili awe ni mfano bora wa kuigwa na wote!

Bikira maria alijiaminisha kwa Mungu

Ni katika muktadha huu, kwa Bikira Maria kukubali mpango wa Mungu, akajikuta akizama katika upweke chanya, akatafakari kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yake, hali yake ya Ubikira, Sheria ya Musa na sasa ujauzito kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hapa anasema Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, imani ilikuwa hatarini sana, lakini Bikira Maria akakubali kupokea yote na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Maisha yake yalikuwa hatarini kwa sababu alionekana kuwa na mimba kabla ya kufunga ndoa. Huu ni upweke ambao ungeweza kumtumbukiza katika ugonjwa wa sonona. Bikira Maria ni shuhuda wa wale ambao hawakuona lakini, wakathubutu kuamini, tofauti kabisa na akina Thomaso, Mtume. Maandiko Mtakatifu yanamtaja Abrahamu kuwa ni mfano bora wa imani katika Agano la Kale. Lakini imani ya Bikira Maria kwa Mungu ilikuwa ni kielelezo cha haki, kwa sababu alimpenda Mungu na kujisadaka kwa furaha bila hata ya kujibakiza! Akawa amemchukua Mtoto Yesu moyoni mwake, hata kabla ya kutungwa kwake mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Bikira Maria alisema “Fiat” badala ya neno “Amina” yaani “na iwe hivyo.” Ikumbukwe kwamba, “Fiat” ni jibu lililokuwa linatumika katika maadhimisho ya Liturujia. “Fiat” yaani “Ndiyo” ya Bikira Maria inaonesha imani na utii kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu, katika hija ya maisha yake hapa ulimwenguni. Huu ni mwaliko pia kwa waamini kufufua na kuiga imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Bikira Maria.

Sherehe hii ilikuwa ikjumuishwa kwenye Kipindi cha Noeli

Kwa njia hii, waamini watakuwa na uwezo wa kuzama katika Maandiko Matakatifu, kupembua: fursa, matatizo na changamoto za maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Hapa kuna haja ya kukazia umuhimu wa imani kama msingi wa matendo yote ambayo Mwenyezi Mungu anatenda kwa wale wanao mwamini Kristo Yesu katika maisha yao. Imani inamwezesha mwamini kujisadaka bila kudai malipo na kwamba, imani ndiyo inayojenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Kumbe, kuna uhusiano wa karibu kati ya neema na imani. Ikumbukwe kwamba, watu wanaokolewa kwa njia ya imani na kutokana na imani, Bikira Maria akapata upendeleo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni imani ya pekee isiyokuwa na kifani na pia ni tendo la kijamii kama Mwenyezi Mungu alivyojifunua mbele yake. Anamtambua Mungu anayejifunua na kutoa ahadi kama ilivyokuwa kwa Abrahamu na kizazi chake. Hili ni fundisho kuu linaloibuliwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu kwamba, imani inamwezesha mwamini kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. (Rej. Rum. 10:10).

Papa Francisko anaibada ya pekee kwa Bikira Maria

Bikira Maria aliamini kwa moyo kiasi kwamba, matendo yake yakawa ni kielelezo makini cha imani tendaji. Kumbe, imani inapaswa kumwilishwa katika maisha ya mtu binafsi pamoja na Kanisa ambamo kuna watakatifu, wafiadini na waungama imani ambao wamewatangulia watu wa Mungu mbele ya haki. Kardinali Raniero Cantalamessa anasema, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, waamini wajifunze kusali kwa ibada na uchaji, ili waweze kuitikia wito wa Mungu bila wasiwasi wala mashaka. Ndiyo yao kama ilivyokuwa ile “Fiat” ya Bikira Maria iwe ni ushuhuda wa kiu na furaha ya Mungu nyoyoni mwao, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo na amani duniani; kwa kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa hakika mwenye haki ataishi kwa imani. Sehemu hii inawahusu hasa wakleri, wanaopaswa kuwa ni watu wa imani, kwa sababu dhamana na utume wao si tu kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kugawa Sakramenti pamoja na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za shughuli za kichungaji, lakini kimsingi wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani katika matendo. Kwa njia hii, wataweza kuwaongoza watu wa Mungu katika uhuru kumwelekea Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Nguvu ya mtu wa Mungu inapimwa kwa njia ya ushuhuda wa imani yake. Bila imani ni vigumu sana kutekeleza dhamana na nyajibu mbalimbali katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwaliko kwa waamini wa kumkimbilia Bikira Maria mwaminifu “Virgo fidelis” ili aweze kuwaombea imani, matumaini na mapendo katika maisha yao!

Bikira Maria

Similar Posts