Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Upendo wa Kiinjili

Na Padre Joseph Luwela – Vatican.

Papa Francisko amesema kwamba, tarehe 8 Desemba 2023 Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Bikira Maria aliamini katika pendo la Mungu na kutoa jibu la “Ndiyo” kwa upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwa Bikira Maria, hali ya kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, ili hatimaye kutangaza na kushuhudia uzuri wa upendo wa Kiinjili.. Mashuhuda wa kiroho na kiutu!

Mababa wa Kanisa wanasema, kwa kuadhimisha katika mzunguko wa Mwaka wa Liturujia ya Kanisa, Kanisa linayaheshimu Mafumbo ya Kristo Yesu. Kanisa humheshimu kwa upendo wa pekee Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa ambaye ameunganika na Mwanaye wa pekee kwa namna isiyoweza kutengwa katika kazi ya wokovu. Tena ndani ya Bikira Maria, Kanisa hustahi na kutukuza tunda bora kabisa kuliko yote la ukombozi, na pia hutazama kwa furaha, kama katika mfano usio na doa yale anayoyatamani na kuyatumaini kwa ajili ya Kanisa zima. Rej. Lumen gentium, 103. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 6 Desemba 2023 wakati wa Katekesi yake kuhusu “Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, tarehe 8 Desemba 2023 Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Bikira Maria aliamini katika pendo la Mungu na kutoa jibu la “Ndiyo” kwa upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwa Bikira Maria, hali ya kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, ili hatimaye kutangaza na kushuhudia uzuri wa upendo wa Kiinjili. Baba Mtakatifu amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwinulia macho yao Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili awasaidie kuwa ni mashuhuda na vyombo vya tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu.

Bikira Maria awe ni faraja na kitulizo kwa watu wanaoteseka kutokana na vita na majanga sehemu mbalimbali za dunia. Waamini wanakumbushwa kwamba, hata wao wamechaguliwa katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili wawe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kuwachagua, ili wafanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo imewaneemesha katika huyo Kristo Yesu. Rej. Efe 1: 4-6. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kukiri imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ni wajenzi wa haki na amani, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili. Waamini wajifunze kujisadaka bila kujibakiza katika huduma, wepesi katika kusikiliza na kutekeleza ushauri kwa ajili ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tangu mwaka 1953, viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki kila tarehe 8 Desemba, wamekuwa na utamaduni wa kwenda kutoa heshima zao kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili iliyoko kati kati ya mji wa Roma.

ikira Maria alipata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama na neema nyingi ili aweze kuwa ni Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Karne kwa karne Mama Kanisa ametambua kwamba, Bikira Maria aliyejazwa neema na Mwenyezi Mungu, alikombolewa tangu mwanzo alipotungwa mimba! Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi wa kwanza wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma na upendo wa Mungu.

Similar Posts