Tafakari Dominika ya IV Kwaresima Mwaka B: Yesu Ni Nuru ya Uzima 2024-10-March
Na Padre Joseph Herman Luwela, – Vatican.Roma-Italia
Leo ni Dominika ya 4 ya Kipindi cha Kwaresima mwaka B. Katika Somo la Kwanza na Injili tutasikia Mungu akiwaonesha watu njia zake kwa namna mbalimbali. Lakini watu hao wanaonekana kutopokea kwa uwazi maelekezo hayo. Ili tuweze kumfuata Mungu aliye mwanga, ya faa tuzitambue njia zake na kuzifuata. Leo pia ni Dominika ya “laetare” maana yake ni Dominika ya furaha. Mwanga wa Mataifa ndiye Kristo Yesu na Kanisa katika Kristo Yesu ni Sakramenti!
afakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu ni nuru halisi na zawadi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. (AFP or licensors)
UTANGULIZI WA JUMLA: Mpendwa msikilizaji na msomaji leo ni Dominika ya 4 ya Kwaresima mwaka B. Katika Somo la Kwanza na Injili tutasikia Mungu akiwaonesha watu njia zake kwa namna mbalimbali. Lakini watu hao wanaonekana kutopokea kwa uwazi maelekezo hayo. Ili tuweze kumfuata Mungu aliye mwanga, ya faa tuzitambue njia zake na kuzifuata. Leo pia ni Dominika ya laetare- maana yake ni Dominika ya furaha. Ndiyo maana wimbo wa kuingilia wa leo unaeleza juu ya furaha, na pia mavazi ya misa kuwa na rangi ya waridi. Hivyo tunafurahi kwa kuwa tumefika nusu ya kipindi hiki cha Kwaresma. Tena tunafurahi kwa sababu tunakaribia kuadhimisha mafumbo makuu ya ukombozi wetu. Yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetuYesu Kristo. Tukiwa na furaha leo tunaalikwa tujitathmini tangu tulipoanza kipindi cha kwaresma kama tunayo mafanikio tuliyoyapata rohoni! Au tunafurahi kwa mazoea tu? Tunafurahi pia kwa vile Mungu ametupa Mwanawe kama Zawadi sababu “jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu…”
Kristo Yesu ni Nuru ya Uzima wa Milele
UFAFANUZI: Wapendwa katika Kristo, kuishi maisha ya giza ni kutoshika maagizo na mafundisho ya Mungu, na hata kama ikitokea tunapokosea, hatupotayari kupokea marekebisho hayo. Na kuishi maisha ya Nurundiyo kufuata mafundisho ya Mungu na kujiweka wazi ili pale tunapoenda kinyume na mafundisho yake tuweze kukubali kurekebishwa.Agano la Kale ni moja ya mfano wa habari inayowaelezea watu kutotimiza maagizo yake. Katika somo la 1 toka ktk kitabu cha 2 cha Mambo ya Nyakati 34:14-16. Tunawaona Waisraeli kwa kutofuata mwanga wa Mungu, waliinajisi nyumba ya Bwana Mungu wa Baba zao, pia walipelekwa utumwani Babeli kwa miaka 70, na hekalu la Yerusalemu kuangamizwa. Kwa hiyo, haya yote yanatokea kutokana na kutenda kwao mambo bila kufuata maelekezo ya Mungu. Ndiyo maana baadaye Waisraeli wanaalikwa kumrudia Mungu kwa maneno haya kama tunavyosoma kaika Kitabu cha Nabii Yoel 2:12 “Lakini hata sasa asema Bwana nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote na kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza Ndiyo kusema, licha ya sisi kukosa uaminifu kwa Mungu, yeye hubaki kuwa mwaminifu daima. Wema wa Mungu kwetu sisi ni wa ajabu, kiuhalisia anaonesha uvumilivu wake wa kutotuacha sisi binadamu. Kwa hakika yeye hachoki kutuhudumia. Yaani anatupa tena nafasi ya kujitazama. Wapendwa, Nuru imetufikia leo kwetu yaani Yesu, kama Injili ya leo isemavyo: “Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele” (Yoh. 3;16) kwa sisi ambao tumeletewa nuru ya Kristo, tunaielekea Nuru hiyo au tunapendelea giza kwa matendo yetu yaliyo maovu. Ndugu zangu, Kristo aliyekuja kwa ajili yetu ni Nuru ya kutuongoza, na zawadi ya Mungu kwetu tukiamua kumfuata Kristo tusiangalie tena mambo ya kidunia yanayotubakisha gizani.
Kristo Yesu ni Nuru ya uzima wa milele
Kristo Yesu ni Nuru ya uzima wa milele
Ingawa aliambiwa na Yesu kuwa “yambidi mtu kuzaliwa mara ya pili ili auone Ufalme wa Mungu” Yoh. 3:3, yaani kubatizwa ili aupate Ufalme wa Mbinguni, lakini alikuwa mashakani, kwakuwa alionekana kuwa bado gizani. Akashindwa kuambatana na Yesu Kristo kwa uwazi na hivyo kubaki kuandamana na mafarisayo wenzake Leo Mwinjili Yohane anatuonesha Zawadi ya Mungu kwetu, Zawadi halisi, nzuri na bora, Zawadi isiyo na masharti, itokayo katika kina cha upendo wa kimungu, upendo wa kibaba unaojali na kukumbatia, upendo usio na chochote nyuma ya pazia, huo watoka kwa Mungu aliye Upendo wenyewe… Zawadi hiyo ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu anayepewa kwetu na Baba, tazama “jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee…” huyo Mwana, hana budi kuinuliwa juu ya mti wa msalaba kama vile Musa alivyomuinua nyoka wa shaba jangwani (Hes 21:8), ili sasa kila mtu aaminie awe na uzima wa milele katika Yeye. Nabii Isaya katika wimbo wa mwanzo anatupa hamasa akisema “furahi Jerusalem, mshangilieni ninyi nyote mumpendao” (66:10). Furaha hiyo ienee leo nafsini mwetu sababu huyo Mwana amekubali na kutii mapenzi ya Baba na kuja ulimwenguni ili sisi tuwe na uzima kisha tuwe nao tele (Yn 10:10). Tuseme nini? Tusali ili Zawadi hiyo itulie kwetu, itende kazi ndani yetu na kutustahilisha uzima ujao. Tufanye nini ndugu zangu? La muhimu ni moja kwa sasa, kumpokea Kristo kama Zawadi ya pekee kwetu. Kama vile waisrael walivyomtazama yule nyoka wa shaba wakapona, nasi tumtazame Kristo Msulibiwa, tutapona! Si tu kuinua macho kutazama na kumuona yuleee, haitoshi. Kumtazama ni kumwamini: “ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele”. Kumtazama Yesu aliyeinuliwa kuna maana ya kumkubali na kumpokea, kumsikiliza na kumfuata, kumtii na kutenda aamuruyo. Kristo anatutazama kwa upendo kutoka juu ya msalaba, anazungumza nasi toka juu ya msalaba, anatupatia vyote kutoka juu ya msalaba, anatukumbatia wote kutoka juu ya msalaba… tumkaribie, tumpokee Yeye aliye zawadi kwetu, tutabarikiwa.
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani
nsi hii Mungu aliupenda ulimwengu…” tuige neno hili na kusema “jinsi hii baba huyu aliipenda familia yake hata akajitoa kabisa kwa ajili ya mke, watoto na ndugu zake… jinsi hii mama aliipenda familia yake hata akajitoa nafsi yake kwa ajili ya mumewe, watoto na ndugu zake… jinsi hii Paroko aliipenda sana Parokia yake hata akajitoa nafsi yake kwa ajili ya waamini wake… jinsi hii wanafunzi waliyapenda sana masomo yao hata wakajitoa kabisa kusoma kwa bidii kwa lengo la kuhudumia jamii ya kesho… jinsi hii wanasiasa waliipenda nchi yao hata wakatanguliza maslahi ya taifa mbele na si maslahi hafifu ya kisiasa tu au yao binafsi, wakiweka kando tofauti na itikadi zao, kuonyeshana utu, kuheshimiana na kushirikiana kuiinua jamii walimo kwa ustawi wa wote katika huduma ya kimapendo… jinsi hii watawala waliwapenda sana raia wao hata wakasikiliza wananchi wao wanataka nini, wakawalinda na kuwahudumia kama Kristo alivyofanya”… kwa matendo na si maneno tu! Sisi tuliokuwa viongozi mbalimbali kadiri ya nafasi zetu (km vile viongozi wa dini, na viongozi wa selikali na sekta binafsi), tunatazamia mageuzi ya ulimwengu ambayo daima yametawaliwa na uovu pamoja na sura mbaya ya mtazamo wa maisha. Na tena kunahofu na mahangaiko juu kuporomoka kwa maadili. Katika hali kama hii, bila kuwa na imani thabiti, ni kuongozwa na hili Nuru ya Mungu ili kuweza kupenya mioyoni mwetu na kufanya mageuzi ya kimaadili hayo na mifumo yote kandamizi ya maisha ya mwanadamu leo.
Kristo ni Nuru halisi na zawadi ya Mungu kwa binadamu
Sisi leo tunahitaji kuwa na imani dhabiti ili kumwamini Kristo Yesu aliye Nuru katika maisha yetu. Sisi leo tuwe na msimamo katika maisha yetu. Tusipende giza na kuchukia nuru, bali tupende nuru ya Mungu kwa kuwa waaminifu katika maeneo yetu mbalimbali ya kazi. Kama viongozi tutekeleze wajibu zetu ipasavyo ktk altare ya Bwana, kama ni ndoa tukae pamoja na familia zetu, wazee tuka pamoja na vijana na kuwaelekeza malezi bora, wanafunzi tusome kwa bidii ili yale tunayoyaelewa yatusaidie kufikia mwanga wa Mungu, watoto wadogo, na wengine, tushike kikweli ukristo wetu, kila mmoja kwa nafasi yake. Tuombe neema ya Mungu tena ili tuweze kuona mwanga wa Mungu unao karibia kujidhihirisha kwetu katika mafumbo makuu ya Pasaka yaani mateso, Kifo, na ufufuko wa Yesu Kristo, na leo tutafakari zaidi kama kweli matendo yetu tunayaelekeza kwa kufuata msingi wa kwaresma. Kama tunajikuta bado hatujitambui basi tufanye tena juhudi zaidi kwa “Kupenda zawadi ya Nuru ambayo ni zawadi ya Mungu kwetu ndiye Kristo Bwana na Mwokozi wetu.”
Nakutakia dominika njema ya furahini-Laetare-
Kibarua wa Kristo-FR Joe