Waraka wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu Kwa Watu wa Mungu
Ujenzi wa umoja na ushirika; wongofu wa kichungaji na kimisionari, ili kutangaza Injili ya Kristo inayosimikwa katika huduma; Upendo wa Kanisa unabubujika kutoka katika Ekaristi. Kanisa linahitaji ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote hasa wale wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni mwaliko wa kuwasikiliza waamini walei na familia na hivyo kuendelea kujikita katika utambuzi wake wa kisinodi na kukuza majadiliano!
Na Askofu Flavian Matindi Kassala, – Vatican.
Mababa wa Sinodi katika Waraka wao kwa watu wa Mungu mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wamejikita katika ushirika, Utamaduni wa ujenzi wa ukimya ili kusikilizana na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na ushirika; wongofu wa kichungaji na kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayosimikwa katika huduma; Upendo wa Kanisa unabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kanisa linahitaji ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote hasa wale wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni mwaliko wa kuwasikiliza waamini walei na familia na kuendelea kujikita katika utambuzi wake wa kisinodi; kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuimarisha mahusiano na mafungamano. Hii ndiyo njia hasa ya Sinodi ambayo Mwenyezi Mungu anaitarajia kutoka kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Kristo Yesu ndiye tumaini la pekee kwa waja wake. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023 anahitimisha rasmi maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Ufuatao ni Waraka wa Kikao cha XVI cha Kawaida cha Sinodi ya Maaskofu kwa watu wa Mungu.