Tafakari Dominika ya Pili ya Mwaka B wa Kanisa: Utakatifu wa Maisha! 14.01.2024
Na. Pd Joseph Luwela-Vatican-Roma
Utakatifu ni mchakato unaowawezesha waamini kuishi upendo katika utimilifu wake kadiri ya nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu. Maisha ya kila mwamini yawe ni kielelezo cha utume kutoka kwa Kristo Yesu anayetaka kuwaletea waja wake mabadiliko katika maisha, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kuambata upendo wa Kristo katika maisha yao. Mama Kanisa anatutafakarisha juu ya mwito wa Mungu kwa mwanadamu.
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya pili ya kipindi cha kawaida cha Mwaka B wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Watakatifu ni watu wanaotia shime pamoja na kuwasindikiza waamini wenzao kama vyombo na mashuhuda wa imani na matumaini kama ilivyokuwa katika Agano la Kale; hata leo hii hawa ni watu wanaoweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki; watu wanaosadaka maisha yao, mashuhuda wa upendo wa Kristo na wale wanaoendelea kujitosa kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Hawa ni majirani wanaotangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku pasi na makuu. Ni watu wanaoshuhudia unyenyekevu katika maisha, kiasi hata cha kuacha alama za mvuto na mashiko katika uekumene wa damu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo Mtakatifu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wewe unaitwa kuwa mtakatifu katika maisha yako kama mtu wa ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu, mfanyakazi na mhudumu wa upendo kwa jirani zako! Neema ya utakaso inaweza kuwasaidia waamini kuambata njia ya utakatifu, kwa kukumbatia Matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini kwa njia ya maisha na ushuhuda wao, wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu: kiroho na kimwili. Wakristo watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani, kumbe, wanatumwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kadiri ya historia na changamoto za Kiinjili; daima kwa kuungana na Kristo Yesu katika Fumbo la maisha na utume wake, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma ya Baba kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu! Utakatifu ni mchakato unaowawezesha waamini kuishi upendo katika utimilifu wake kadiri ya nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu. Maisha ya kila mwamini yawe ni kielelezo cha utume kutoka kwa Kristo Yesu anayetaka kuwaletea waja wake mabadiliko katika maisha, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kuambata upendo wa Kristo katika maisha yao. Mama Kanisa Mtakatifu leo katika masomo aliyoyachagua anatutafakarisha juu ya mwito wa Mungu kwa mwanadamu. Mungu anamwita kila mmoja wetu kwa namna mbalimbali na anataka sote tuitike vizuri wito huo, tudumu kiaminifu katika wito huo na mwisho tuweze kufika kwake yeye aliye Mtakatifu. Basi leo tuombe neema yake itusaidie tuweze kuisikia vizuri sauti yake inayoita na kuifuata. Pamoja tuongozwe na wazo hili “tusikie sauti ya Mungu na kutenda tuyasikiayo.”
UFAFANUZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji wa tafakari zetu, kama nilivyotangulia kusema mwanzo katika utangulizi ya kwamba Mungu wetu ni Mungu anayeita; naye huita watu kwa lengo au malengo mahususi. Ndio kusema Mungu ana mpango na maisha ya kila mmoja wetu. Kuna kitu ambacho anataka kukitekeleza kupitia zawadi ya maisha aliyompatia kila mmoja wetu. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa tupo hapa duniani kwa sababu fulani muhimu na maalum. Hata hivyo, si kila mara tunatambua mara moja sababu ya uwepo wetu na wa wenzetu hapa duniani, au uwepo wetu mahali fulani, katika mazingira fulani, katika hali fulani kwa wakati fulani. Hivyo, tunahitaji mwongozo kuweza kuyatambua hayo ndio maana mama kanisa kama Sakramenti ya wokovu huendelea kuwakumbusha watoto wake na watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kuwa Mungu anawapenda na daima yupo tayari kuwaokoa kama wataendelea kuisikia sauti yake na kuitii. Masomo yetu yote tuliyoyasikia yanatanabaisha na kuoensha wazi na vizuri kabisa dhamira hii ya mwito anaoutoa Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu. Katika somo la kwanza tumesikia jinsi Mungu anavyomuita mtoto Samueli. Mungu alikuwa na mpango na maisha ya Samueli tangu akiwa mtoto mdogo. Yeye alimwita awe nabii na mwamuzi wa mwisho katika Israeli. Kwa msaada wa kimaongozi ya mzee Eli, Samueli aliweza kuitambua sauti ya Mungu, kuiitikia vizuri na kudumu katika wito aliokuwa ameitwa na Mungu hata “watu wote kote nchini Israeli toka Dani, upande wa kaskazini, hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wakajua kuwa Samueli alikuwa nabii mwaminifu wa Mwenyezi-Mungu” (1 Sam 3:20). Samueli anatukumbusha hitaji la msingi sana katika mahusiano yaani mahusiano kati ya Mungu na watu wake yaani sisi wanadamu na mahusiano ya sisi kwa sisi katika nyanja zote za maisha, ni ukweli usio na mashaka kuwa pale inapodhaniwa na kudhibitika kuwa hakuna uaminifu katika mahusiano na utendaji wowote imani, matumaini na yatarajiwayo mazuri hutoweka, huzuini na maumivu hutawala kwani uhakika wa haki huingia dosari kubwa na kupatikana kwa amani hufifia kama si kukanyagwa kwani msingi wa yote haya ujengwa katika fadhila ya uaminifu ambamo ndanimo upo upendo wa baba na mwana na kaka na dada.
Mawazo tuliyosikia somo la kwanza yanajikamilisha katika Injili ya leo. Yohane Mbatizaji anakuwa ni msaada kwa watu waliotaka kumfuata Masiha. Yohane, kwa mahubiri na ubatizo wake wa toba, aliwaandaa watu kumpokea Masiya na tukumbuke Yohane mbatizaji leo ndio mama kanisa mtakatifu anaendelea na utume huwa wa kuwafundisha watu na kuwabatiza kuwafanya wana na wateule wa Mungu. Ikumbukwe Kati ya hao walikuwapo wanafunzi wake ambao baadaye walikuja kuwa wafuasi wa kwanza wa Yesu Kristo hata leo ndio tumaini la kanisa kuwa wabatizwa waendelee kuwa wamisianari na wafuasi wa Kristo Bwana na mwalimu wetu. Hao walijazwa kiu na hamu ya kutaka kumjua Masiya na kuambatana naye. Kwa msaada wa Yohane Mbatizaji, mwalimu wao, wanaweza kumtambua Masiya na kumfuata. Kama vile mzee Eli alivyomwongoza mtoto Samueli kuitambua sauti ya Mungu na kuitika, vivyo hivyo Yohane Mbatizaji anawaongoza wanafunzi wake hata wanamtambua na kumfuata Masiya; nao wakadumu kiaminifu katika hilo maisha yao yote. Hata sasa mama kanisa hachoki kufanya hivyo swali je wewe msomaji na msikilizaji mkristo mwenzagu unatekeleza hilo kiaminifu? Katika somo la pili Mtume Paulo anatuhimiza juu ya kujilea katika utakatifu kwa kuwa tuliumbwa katika sura na mfano wa Mungu aliye Mtakatifu na sisi ni mali yake. Kwa kweli, somo hili linaweka mkazo juu ya kuwa waaminifu kwa mwito tulioupokea kutoka kwa Mungu na linatuhimiza kutumia vizuri vitu tulivyonavyo na hasa miili yetu kwa ajili ya Bwana anayetuita kwake. Hii ni mbinu anayotupatia Mtume Paulo ili kutusaidia sisi kutokupoteza dira katika kuitikia wito wa Mungu ndio maana anatuhasa tuikimbie dhambi maana hiyo itatutia najisi na kutupotosha zaidi inatuweka mbali na Mungu wetu anayetupenda upeo, tunaondolewa neema ya utakaso kwani twafahamu faida ya kuwa na karibu na kitu kizuri kama waswahili wasemayo “ ukikaa karibu na walidi utanukia kama ua la walidi” hiyo tukiwa karibu na Mungu kwa matendo na maneno yetu mema kadiri ya mapenzi na maagizo yake tutaendelea kujizingilisha katika ukamilifu kwani yeye ni Mkamilifu.
Mpendwa sikilizaji na msomaji, tukiwa bado mwanzoni kabisa mwa mwaka 2024 mwaka wwa serikali na pia bado tupo mwanzoni kwa mwaka wa liturujia japo tumeanza tangu majilio, ila sasa ni dominika ya pili ya mwaka kipindi cha kawaida, ninaamini kabisa ya kwamba masomo ya leo yamekuja kwa wakati sahihi maana yanatupatia sisi fursa ya kujiuliza na kujitafakari vizuri juu ya miito yetu mbalimbali ambapo kila mmoja amaitwa kwa namna yake. Mwanzo huu ni fursa nzuri ya kujitafakari. Hebu tunapojitafakari kuhusu maisha yetu na mwito tunaoupokea kutoka kwa Mungu, tutumie swali lile ambalo Yesu aliwauliza wale wafuasi: “Mnatafuta nini?” Kila mmoja wetu anaitwa na Mungu kwa namna yake na kwa mazingira yake. Sina shaka kwamba kwa msaada na miongozo ya wazazi, walezi, ndugu, jamaa, marafiki na watu wote wenye mapenzi mema sisi sote iwe ni mapadre, mashemasi, mtawa, mseminari, au watu wa ndoa, watu wa kada mbalimbali katika jamii zetu, tulisikia sauti au mwito wa Mungu na tukaitika. Lakini je, tunajua nini tunakitafuta hata baada ya kuwa tumeitikia mwito huo wa Mungu? Haitoshi tu kuwa padre, shemasi, mtawa ,msiminari, baba au mama wa familia, mwanafunzi, mwalimu, mkulima, mfanyakazi, raisi, waziri au mtu yeyote yule. Hivyo vitabaki kuwa vyeo vya sifa kama hatutajua nini tunakitafuta katika yote hayo. Sasa je, tunavijua vipaumbele vyetu? Tunapaswa kutambua ya kwamba Mungu haiti mara moja tu. La hasha! bali sauti yake huendelea kusikika tena na tena ili kutusaidia sisi kudumu kiaminifu katika wito ambao yeye ametuita. Mungu huita tena na tena kupitia watu, wakati au matukio mbalimbali katika maisha yetu. Kwa upande wetu sisi tunadaiwa usikivu na u-tayari wa kuongozwa kupitia watu, wakati na matukio kwani Mungu anaongea nasi wakati wote kwa njia nyingi na taofauti.
Maisha ya mwanadamu yana maana pale yanapokuwa na dira, yaani pale tunapotambua nini tunapaswa kukifanya na tukaenenda kadiri ya hilo tunalopaswa kulifanya basi maisha yetu yanapata maana. Kama unaishi pasipo dira/mpango basi uko hatarini maana unapoteza muda na nguvu zako bure na mwisho wa siku ni hasara. Kitu chochote kikifanyika bila ya kuwa na mpango mwisho wa siku kitakuwa kibaya tu. Maisha yetu ni mafupi na hatujui yataisha lini, hivyo basi tusipoteze muda wetu kujihangaisha na mambo ambayo si vipaumbele vyetu. (Mfano kukaa kulalamika bila kuchukua hatua za kutatua changamoto zilizo mbele yako iwe ni kiongozi wa dini au serikali, baba au mama wa familia, mwanafunzi , mfanyakazi, mfanya biashara nk) Aidha, wajibu tulio nao sisi sote ni kuongozana sisi kwa sisi katika njia zilizo sahihi zitakazotufikisha kwa Mungu. Wewe ukiwa ni mzazi unao wajibu wako: “Mfunze mtoto namna ya kuishi vizuri, naye hatasahau njia hiyo hata uzeeni” (Mit 22:6). Hata tukiwa katika sehemu zetu za utume, kazi, malezi na mafunzo, na popote pale tunapotakiwa kuwajibikiana, tunapaswa kusaidiana na kuongozana. Kila mmoja aone ya kwamba anawajibika kwa ustawi wa mwingine na ahakikishe ya kwamba mwingine analifikia lengo ambalo Mungu amemuitia.
ATIMA: Basi tukiwa na utambuzi huo ya kwamba Mungu ametuita, tunapaswa kutumia vizuri kila kitu tulicho nacho, iwe ni muda, afya njema, akili, nguvu na mengine mengi tunayojaliwa naye ili tuweze kuitikia vizuri mwito wake na kuwa waaminifu kwa mwito huo. Juu ya yote hayo lazima kuyaratibu maisha yetu vizuri na kuyapa dira. Kuvijua vipaumbele vyetu ni muhimu katika kulifikia lengo. Nakutakia dominika njema ya kusikia sauti ya Mungu na kutenda yale tusikiayo kutoka kwake na mwisho tuambiwe vyema mtumishi mwaminfu ingia ufurahi na bwana wako hapo tutafurahia matunda ya uaminifu wetu.